Warumi 6 inahusu ukombozi kutokana na nguvu ya dhambi. Ili tuweze kuelewa toba na ushindi, ni lazima tuelewe dhambi ni nini.
► Dhambi ni nini?
Kwa kawaida Biblia huzungumzia kuhusu matendo ya dhambi kama yanayofanywa kwa hiari (1 Yohane 3:4-9, Yakobo 4:17). Wakati mtu anapofanya kwa kukusudia na kwa kujua akachagua kutokumtii Mungu, hiyo ni dhambi ya kujitakia au hiari.
Kuna utendaji wa bila kufahamu au ukiukaji wa bahati mbaya wa sheria ya Mungu hauvunji sheria au uhusiano na Mungu kama dhambi ya kukusudia inavyofanya. Tunapokuwa tunatembea kwenye nuru (tukiishi kulingana na ukweli tunaoujua), tunatakaswa na aina zote za dhambi (1 Yohane 1:7) na haihitajiki kuwa kwenye mashaka kwamba ukiukaji unaofanyika kwa bahati mbaya utatutenganisha na Mungu.
Kimsingi kifungu hiki kinazungumzia kuhusu dhambi za kujitakia au za hiari, ambazo huharibu Imani na kuleta madhara katika uhusiano wa mtu na.
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu ya 4, kifungu cha 1
Sehemu ya 4 ya Warumi (Warumi 6-8) inahusu utakaso wa wale waliohesabiwa haki.
Hadi kufikia hatua hii, Paulo alikuwa anazungumzia kuhusu haki iliyoingizwa ndani. Haki hii inaingizwa kwa neema wakati wa kuhesabiwa haki na ina maana kuwa mwamini anakuwa mwenye haki kweli kwa kuwa huru kutoka nguvu za dhambi na anasaidiwa na Roho Makatifu kuishi maisha matakatifu. Kwa hiyo, Mwamini sio tu anahesabiwa kuwa mtakatifu, lakini anafanywa kuwa mtakatifu haswa. Hii huitwa utakaso.
Kwenye somo hili tutajifunza Warumi 6, ambayo ni ushindi dhidi ya dhambi.
Jambo Kuu katika sura ya 6
Mtu aliyeamini yuko huru kutokana na utumwa wa dhambi na ni lazima achague kuishi kwa ushindi dhidi ya dhambi na kwa utii kwa Mungu, asije akarudia tena kuwa chini ya udhibiti wa dhambi.
Muhtasari wa sura ya 6
Warumi 6 ni majibu ya Paulo kwa dhana potofu waliyonayo watu: dhana potofu ni kwamba kwasababu ya neema, waamini hawahitaji kuishi katika utii wa sheria za Mungu. Kosa hili linatokana na uelewa mbaya wa neema. Paulo anasahihisha kosa hili kwa kuuliza na kujibu maswali mawili yanayodhaniwa (6:1,15).
Baadhi ya watu wanaposoma 5:20, wanafikiri kuwa wanapaswa kuendelea katika dhambi, ili kwamba tuwe na neema zaidi (6:1). Inaonekana wanafikiri kuwa, kwa kuwa kumbukumbu za dhambi zetu zimebadilishana na haki ya kupewa, basi haina shida kama tukiendelea kufanya dhambi.
Kuna sababu nyingine ambayo baadhi ya watu hufikiri kwamba waamini hawahitaji kuishi katika utii wa sheria za Mungu. Wanasema kuwa tumekubaliwa kwa neema na sio kwa matendo. Hii ni sababu inayowafanya kukosea kufikiri kuwa chochote tunachofanya hakuna shida (6:15).
Paulo anakataa kwa nguvu zote maswali ya dhana hizo. Anajibu kwa kutao ufanfanuzi kuonyesha kuwa ushindi dhidi ya dhambi ni muhimu.
► Mwanafunzi atapaswa asome Warumi 6 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo ya Aya-kwa-Aya
(6:1) Hapa mtume aliuliza swali ambalo mtu anaweza akauliza baada ya kuwa ameshasikia kwamba neema ilikuwa nyingi zaidi kuliko dhambi. Mtu anaweza kufikiri kwamba dhambi kwa uhakika inaleta matokeo mazuri kwa sababu inaleta neema zaidi. Kwa wazo hili ni kuwa tuko huru kuishi kiholela katika dhambi.
(6:2) Mtume anatoa majibu ya swali hilo kwa namna ya kukasirika. Kisha analitolea ufafanuzi kwamba haiwezekani tena sisi tuendelee kuishi kwenye dhambi, kwa sababu tayari tulishaifia dhambi.
(6:3-5) Hatuendelei kuwa kwenye dhambi kwa sababu tumeunganishwa pamoja na Kristo katika mfano wa mauti yake na kufufuka kwake. Kama Warumi 5:15-19 inavyoeleza, Yesu alikamilisha kazi ya ukombozi kwa ajili yetu sisi sote. Kwa imani tunaunganishwa pamoja naye, ili kwamba upendeleo wa Mungu uweze kuendelezwa kwetu kama ilivyo kwa Kristo.
Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi mara moja tu, na kisha anaishi kwa ajili ya Mungu. Kifo cha Yesu kilikuwa ni kwa ajili ya dhambi zetu na siyo kwa ajili yake mwenyewe, lakini jambo muhimu hapa ni kwamba suala la dhambi lilifikishwa mwisho. Kwa imani, tumekufa na kufufuka pamoja na Kristo; ili kwamba na sisi pia tuwe tumefikia mwisho wa kuishi dhambi.
Ubatizo ni tendo la kuonyesha kifo cha Yesu na kufufuka kwake, ikiashiria ushiriki wetu katika hayo.
(6:6) Utu wa kale unawakilisha hali na maisha ya dhambi kabla ya kuokoka. (Sehemu nyingine ya baadaye katika somo hili inaelezea dhana ya “Utu wa Kale”) Maisha ya dhambi yamemalizwa kabisa, kwahiyo sisi siyo watumwa wa kutumikia dhambi tena.
Tambua maneno yaliyotumika katika kifungu hiki kuhusiana na kile kilichofanyika dhidi ya dhambi: imekufa, ilisulubiwa, na iliharibiwa. Maneno yanaunganisha ushindi kamili dhidi au juu ya dhambi.
(6:7-11) Msisitizo katika aya hizi ni kwamba udhibiti wa dhambi umekwisha kwa mtu aliyeamini. Kielelezo hapa ni kifo. Mtu aliye mfu yuko ameshida dhambi, na tunapaswa tuwe na uzoefu wa kiroho ambao unafanana na kifo.
Baada ya kufufuka, Yesu hakufa tena na hataendelea kufa tena. Alimalizana na kifo. Tunapaswa tufe kabisa juu ya dhambi na kumalizana nazo na kisha tuwe huru dhidi ya hiyo dhambi. Kifo katika dhambi ni suala la kumalizika kwa haraka, kisha tunaendelea kuishi kwa ajili ya Mungu.
Muunganiko wa Mkristo na kifo cha Kristo kwa dhambi, kuzikwa kwake, na baadaye kufufuka ambako Paulo alielezea katika Warumi 6:1-23 kunamweka Mkristo huru kutokana na nguvu na utumwa wa dhambi. Anakuwa ametangazwa kuwa mfu katika dhambi (Warumi 6:2) na kuwekwa huru kutokana nayo (Warumi 6:7). Kuwa mfu katika dhambi ni kutokuwa tena chini ya nguvu za dhambi au kuthibitiwa nayo. Kwa Imani mwamini lazima kujifikiria kuwa mfu katika dhambi, lakini aliye hai kwa Mungu katika Yesu Kristo. (Warumi 6:11). Hii inamaanisha kwamba Mkristo anapaswa awe na uzoefu wake binafsi katika kile ambacho Mungu anatangaza kwamba ni cha ukweli kuhusiana na yeye. Hapaswi kutoa mwanya kwa dhambi kuendelea kutawala tena ndani ya mwili wake (Warumi 6:12), au kuvitoa viungo vya mwili wake kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi (Warumi 6:13a). Badala yake, anapaswa ajitoe mwenyewe kama dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu (Warumi 12:1), na kuvitumia viungo vya mwili wake kuwa silaha za haki. (Warumi 6:13, 19).[1]
Katika Warumi 6:11 neno “Hesabu” ni neno la uhasibu. Ni kuthibitisha kitu ambacho ni cha ukweli. Siyo tamko la kujifanya. Mtume hawaelezi waamini waseme kitu ambacho siyo cha ukweli. Mtu aliyeamini anapaswa atambue kwamba amekombolewa kabisa kutokana na dhambi kama kwamba amekufa, na anapaswa achague kuishi kwenye uhuru kamili dhidi ya nguvu ya dhambi.
► Je, inamaanisha nini kujihesabu umekufa katika dhambi?
Sehemu iliyobakia ya sura hii inaelezea sababu nyingine kwamba ushindi dhidi ya dhambi ni jambo muhimu. Sisi siyo watumwa wa kufanya dhambi, bali watumishi wa Mungu. Huwezi kutumikia dhambi na Mungu kwa wakati mmoja. Ulipokuwa mtumishi wa dhambi, hukufanya uadilifu (6:20). Kwa sasa uko huru na dhambi na ni mtumishi wa Mungu; kwa hiyo, unaishi katika utakatifu (6:22).
(6:12-13) Hapa tunaona ulinganifu. Kama hatuwezi kuwa na ushindi dhidi ya dhambi, dhambi itatutawala. Waamini hawatawaliwi na tamaa za dhambi. Kutumia mwili wako kwa ajili ya matendo ya uovu ni sawa na kuutoa uwe kwenye mamlaka ya dhambi. Badala yake, mwili wako ni mali ya Mungu na unapaswa utumike kwa ajili yake.
(6:14) Kuwa chini ya sheria ina maana kuwa unategemea kuitii sheria ili ukubaliwe na Mungu. Mtu huyo hana neema inayookoa, kwa hiyo, anahukumiwa katika misingi ya matendo. Kwa kuwa hakuna mtu yeyote asiye na neema anaweza kuishi kwa kuishinda dhambi, kuwa chini ya sheria ina maana umehukumiwa na uko chini ya nguvu ya dhambi. Kuwa chini ya neema ina maana kuwa unategemea neema ili kukubaliwa na Mungu. Mtu aliye chini ya neema hayuko chini ya nguvu ya dhambi. Aidha Kuwa chini ya sheria au chini ya neema haisemi ni Agano la Kale au Agano Jipya.
► Watake wanafunzi waelezee tena inamaanisha nini kuwa chini ya sheria.
(6:15) Hapa mtume aliuliza swali ambalo mtu anaweza kuuliza baada ya kusikia kwamba hatuko chini ya sheria: "Je, tunaweza kutenda dhambi, kwa sababu hatuko chini ya sheria?” Mtu anafikiri kwamba kama kukubaliwa kwetu mbele za Mungu sio kwa utii wetu basi utiifu si wa muhimu. Paulo anajibu swali hili kwa uzito mkubwa.
Paulo hakuelezea moja kwa moja ni kwa nini neema haifuniki dhambi zinazoendelea kufanywa. Badala yake anaelezea kwamba mtu hawezi kuwa mtumishi wa Mungu kama yuko chini ya nguvu ya dhambi.
(6:16) Haiwezekani kutumikia kwa pamoja Mungu na dhambi kwa sababu wewe ni mtumishi kwa yule unayemtii. Kama utaitii dhambi, dhambi ndiyo bwana wako; ikiwa na maana kwamba Mungu siyo Bwana wako. Kama mtume Petro alivyosema, kwamba mtu akishindwa na mtu basi aliyeshindwa huwa mtumwa wa mtu yule” (2 Peter 2:19). Huwezi ukajiachilia kwa dhambi bila ya kuwa mtumwa wa dhambi.
(6:17-18) Waamini wamekombolewa kutoka katika nguvu ya dhambi na sasa wanaitumikia haki. Walipata ukombozi huu kwa kuitii injili. Pia, imeelezwa kwamba kuitumikia haki ilikuwa ni muhimu kwao kukombolewa kutokana na dhambi.
Sura yote inaelezea ulinganifu kati ya kifungo cha dhambi na kuishi ya maisha ushindi. Kamwe hakuna wazo kwamba inawezekana kwa mtu aliyeamini kuwa chini ya nguvu ya dhambi au kwa mwenye dhambi kuwa mwenye haki wakati anaendelea kutenda dhambi. Itakuwa ni vigumu kupata njia ambayo Paulo angeweza kusemea jambo hili kwa njia iliyo hakika zaidi.
(6:19) Alisema kwamba analisemea hili kwa jinsi ya kibinadamu ili kwamba waweze kulielewa. Hapo mwanzo walijiachilia kwa ajili ya kutumikia dhambi, ambako kuliwaingiza ndani zaidi katika kutenda dhambi. Sasa, wanapaswa wawe wenye haki katika matendo yao, jambo ambalo ni muhimu kwa ajili ya utakatifu. Mtu hawi mtakatifu kwa kutenda mambo ya haki, lakini pia siyo mtakatifu kama hatendi mambo ya haki.
► Je ni kwa jinsi gani unaweza kuelezea isivyowezekana kumtumikia Mungu na kuishi katika dhambi kwa wakati mmoja?
(6:21-23) Dhambi haileti faida yeyote lakini yenyewe mwisho wake ni kifo. Mwenye dhambi huchuma mauti; kifo ni mshahara wa dhambi. Mwamini hapati uzima wa milele kwa kuufanyia kazi, lakini huupokea kama kipawa cha neema.
Wengine wanafikiri kuwa wakati mtu binafsi amemkubali Kristo wokovu wake uko salama bila matatizo hata wakati ambapo aina ya maisha yake yanajichanganya kabisa na anavyosema.[1] Hata wakati ambapo madai ya wokovu bado hayajaanza kutenda kazi katika kuleta mabadiliko ya maisha; hata wakati ambapo hakuna tunda la toba na kuokoka kunakoonekana; na hata wakati ambapo mtu anakataa kuwa mwanafunzi wa kweli wa Yesu, anaweza kuwa amekiri wokovu kwa kudanganya. Huu ni udanganyifu wa kiwango cha juu sana na unapingwa na maandiko mengi.
Na tukaribie wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya, tumeoshwa miili kwa maji safi (Waebrania 10:22).
Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho (1 Petro 1:5).
Kutokana na vifungu hivi tunajifunza kwamba uhakika wa kibiblia wa wokovu unategemea imani:
Uhakika wa wokovu unategemea imani ambayo huelewa “uhakika kamili.” Uhakika huanza na ufahamu ulio wazi wa injili
(1 Wakorintho 15:3-4). Haya ndiyo “maarifa kuhusiana na uhakika” ambayo yamezungumziwa pia katika Wakolosai 2:2. Wokovu ni kwa neema peke yake, kupitia imani iliyo katika kifo kilichochukua nafasi mbadala cha Yesu Kristo kwa niaba yetu (Waefeso 2:8-9). Hitaji la wokovu siyo ukamilifu usio na dhambi (hakuna mtu atakayestahili) au kujisikia umeokoka wakati wote, lakini afadhali kuaminika mara kwa mara katika sifa ya Kristo na kazi ya ukombozi iliyokamilishwa hata wakati tunapojikuta tumeanguka. Hamu ya kuwa mwaminifu itafuata imani inayookoa iliyo halisi.
Uhakika wa wokovu unategemea imani ya dhati – “moyo wa kweli.” Mtu aliyeokoka kwa dhati ni yule ambaye “ameoshwa kutokana na dhamiri ya uovu” (Waebrania 10:22). Hatia na aibu vimeondolewa na kubadilishwa kwa amani na upendo. Mtu aliyeokoka kwa dhati ni yule pia ambaye mwili wake “umetakaswa kwa maji yaliyo safi” kwa kuwa ya kale yamepita tazama, yamekuwa mapya (2 Wakorintho 5:17). Mtu aliyeokoka kwa dhati ni yule pia ambaye hukubali na huyakiri makosa yake na dhambi ili apate kusamehewa na kuwekwa huru (Mathayo 6:12, Yakobo 5:16).
Uhakika una masharti yake kwenye imani iliyo hai – “kwa nguvu za Mungu wanaongozwa kupitia imani” maana yake ni kama vile ulinzi ulipo katika kasiri au ngome. Nguvu ya kiungu inalinda, inahifadhi, na mwisho wake itatuongoza kwenye ushindi. Ni nguvu ya utakaso inayotokana na damu ya Kristo na nguvu ya kufufuka kwake ambayo tunaipata kwa njia ya imani na kwamba inahifadhi roho zetu katika uzima wa milele. Imani peke ya kweli inayookoa; imani ambayo inaendelea katika Kristo na katika kazi yake aliyoikamilisha msalabani. Imani siyo kazi, ni sharti kwa ajili ya wokovu. Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anasema hivi: “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza” (Waebrania 11:6).
Watu wengi wanaamini kwamba kufungamanisha masharti yeyote kwenye wokovu ni kushika sheria, lakini Yesu na kila mwandishi kwenye Agano Jipya kwa uwazi kabisa walifundisha kuhusu umuhimu wa imani endelevu.
Ninyimkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli (Yohane 8:31).
Mkidumu tu katika ile imani, hali mmewekwa juu ya msingi, mkawa imara; msipogeuzwa na kuliacha tumaini la Injili… (Wakolosai 1:23).
Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye (Waebrania 10:38).
Uwe mwenye imani na dhamiri njema, ambayo wengine wameisukumia mbali, wakaangamia (1 Timotheo 1:19).
Akielezea uhakika wa wokovu, John Wesley alisema,
Faraja yangu haitegemei maoni yoyote, iwe muumini anaweza au hawezi kuanguka, wala haitegemei kumbukumbu ya chochote kilichofanyika ndani yangu jana; bali inategemea kile kilichopo leo, katika kumjua kwangu Mungu leo ndani ya Kristo, akinipatanisha na yeye mwenyewe; kwa sasa ninapoona nuru ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo; nikitembea katika nuru kama yeye alivyo katika nuru, na kuwa na ushirika na Baba na Mwana. Faraja yangu ni kwamba kwa neema ninaweza kumwamini Bwana Yesu Kristo, na Roho Mtakatifu anashuhudia pamoja na roho yangu kwamba mimi ni mtoto wa Mungu.[2]
► Kutokana na dhana zilizoko katika sehemu iliyotangulia, nawezaje kuelezea kwamba Mkristo anaweza kuwa na uhakika wa wokovu ulio katika msingi wa imani iliyo hai?
[2]John Wesley, “Serious Thoughts Upon the Perseverance of the Saints”, in The Works of John Wesley: Letters, Essays, Dialogs and Addresses Vol. X, (Grand Rapids, MI: Zondervan) 295. Pia inapatikana mtandaoni kupitia: https://archive.org/details/worksofjohnwesle0010wesl/
Utu wa Kale
Neno utu wa kale limejitokeza mara tatu katika nyaraka. Kwa mara zote tatu linatumiwa na Paulo. Kwa kulinganisha haya matukio matatu katika muktadha wake tunaweza tukaona neno hili linamaanisha nini.
Wakolosai 3:9
Wakolosai 3:9-10a panasema,“ “Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; mkivaa utu mpya, …” Paulo alisema kwamba waamini hawa walikuwa tayari wameshauvua utu wa kale. Hakuwa amemaanisha kwamba walikuwa tayari wameshatakaswa kabisa, kwa sababu mengi yaliyoko katika Wakolosai 3 ni wito kwao kwa ajili ya utakatifu.
Mwanzoni alikuwa amewaambia waamini wa Kolosai kwamba, "Yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko... Yafikirini yaliyo juu... Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu" (Wakolosai 3:1-3) Aliendelea kusema, "Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya..." (3:5). 3:6 inasema dhambi kama hizo zitaleta hukumu ya Mungu, na 3:7 inasema kwamba waamini hawa hapo nyuma walifanya mambo haya. Paulo anadai kuwa hawavumilii mambo kama hayo katika maisha yao kabisa. Hii inaoneshwa katika maelezo kuwa wanapaswa kufisha vitu vyote hivi.
Kisha, aliwataka wayaweke mbali yote yale: hasira, na ghadhabu, na uovu, na matusi vinywani mwao (3:8). Haya yote hayaendani na maisha katika Kristo.
Kisha tunakuja kwenye taarifa kwamba wanapaswa wayafanye haya yote kwa sababu tayari walishauweka nje utu wa kale pamoja na matendo yake yote.
Anawataka kuendelea katika imani ya kikikristo kwa kuelezea tabia ya utakatifu (3:12), kisha kwa kuhimiza kufanana na Kristo katika mahusiano (3:13), kisha akawaeleza wawe na upendo, ambao hufunga kila kitu pamoja katika ukamilifu (3:14).
Inaonekana wazi kwamba katika muktadha huu utu wa kale ulikuwa ni maisha ya kale yaliyoachwa wakati wa kuokoka. Kwa kuwa walishafanya hivyo, Paulo aliamini kwamba wanaweza wakaendelea kukamilika kabisa kwenye utakatifu.
Waefeso 4:22
Mstari huu uko kwenye kifungu ambacho kinaenda sambamba na kifungu kingine kilichoko katika Wakolosai. Katika 4:17-19, anaelezea mfumo wa maisha ya Wamataifa; kisha kwenye 4:20 akalinganisha na maisha ya mtu aliyeamini. 4:21-24 zinaelezea inamaanisha nini kuwa “umejifunza Kristo” (4:20) na kuwa umemsikia na kufundishwa katika yeye (4:21). Mambo haya yote yanahusisha kuachana na utu wa kale na kuvaa utu mpya. Hii ni sehemu ya kile kilichokuwa kimetokea wakati walipookoka.
Kifungu hiki katika Waefeso kinafuata mpangilio sawa na ulioko katika Wakolosai 3. Baada ya taarifa kwamba kuachana na utu wa kale ni sehemu ya injili waliyokuwa tayari wameshajifunza, agizo la kwanza la Paulo kwao ni kwamba waachane na uongo. Akaendelea kutaja uchungu wote na ghadhabu, hasira, kelele, matukano pamoja na kila namna ya ubaya. Aliwaagiza wawe wema na wenye kusamehe. Mambo haya yote pia yametajwa katika Wakolosai baada ya maelezo kwamba walishaachana na utu wa kale.
Utu wa kale siyo kitu ambacho mtu aliyeamini anahitaji kuachana nacho, bali ni kitu ambacho kiliondoka wakati ule wa kuamini na kuokoka. Walikuwa bado hawajawa watakatifu kabisa, na Paulo aliwataka wakamilishe utakatifu wao katika maisha yao ambao utakuwa sawa na mwanzo waliokuwa wameuanzisha wakati walipoachana na utu wa kale.
Warumi 6:6
Katika kifungu hiki Paulo anaonyesha tofauti kubwa iliyopo kati ya mwenye dhambi na mtu aliyeamini. Jambo kuu katika sura hii ni kuwathibitishia mfuasi wa Yesu kuwa anayo ushindi dhidi ya dhambi. Moja ya sababu alizitoa kuthibitisha kwamba mtu aliyeamini anaweza kuishi maisha yenye ushindi dhidi ya dhambi ni kwamba utu wa kale umesulibiwa. “mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena.” Hapa ni wazi anasema kwamba mtu aliyeamini yuko huru mbali na dhambi kwa sababu ya kile kitu ambacho tayari kilishatendeka wakati wa kuamini na kuokoka.
Hitimisho
Kwa hiyo neno utu wa kale linamaanisha nini? Utu wa kale ni maisha ya kibinafsi ya dhambi ambayo mwenye dhambi anaachana nayo wakati anapokuwa ameamini na kuokoka.
Mtu mpya anapookoka anakuwa bado ana tabia na mwenendo ambavyo ni sawa zaidi na utu wa kale kuliko utu mpya. Hii ndio maana Paulo aliwaambia waamini kuendelea kufanya matengenezo katika maisha yao ambayo yatakwenda sawa na kule kuukataa utu wa kale. Alikuwa anasema, “Kwa kuwa umeachana na maisha ya zamani ya dhambi, unahitajika uachane na tabia yeyote ambayo haiendani na maisha mapya ya haki.”
Kujitoa kwa Yesu kwa ajili ya Utakaso wetu.
Katika Warumi 6:1-10 tunaelezwa kuhusu kujitoa kwa Yesu kwa ajili ya Utakaso wetu binafsi.[1] Tulipokuwa tumezaliwa mara ya pili, tuliwekwa ndani ya Kristo. Kile chote alichokifia na kufufuka tena ili kukikamilisha kilifanyika chetu katika yake. Hii inamaanisha kwamba katika Kristo tunavyo rasilimali ya ushindi kamili dhidi au juu ya dhambi.
Kwa sababu ya muunganiko wetu na Kristo, lolote lililotokea kwake lilikuwa limetokea pia kwangu. Alipokufa, na mimi nilikufa. Alipofufuka, na mimi nilifufuka ndani yake. Kwa sababu ya muunganiko huu ulio hai pamoja na Kristo, mtu aliyeamini ana uhusiano mpya kabisa katika dhambi. Kwa sasa tumekufa kwa dhambi. Tumekufa kwa pamoja kwenye matendo ya dhambi pamoja na kanuni ya dhambi. Huu ndio msimamo wa uhusiano wetu katika dhambi.
Kutokana na muungano wetu na Kristo, kwa sasa tunatembea katika upya wa maisha kwa sababu tunashiriki maisha yake ya ufufuo.
Kutokana na muungano wetu na Kristo, kusulubishwa kwake kunakuwa ni kusulubishwa kwangu. Kwa kuwa kifo chake kulishinda nguvu ya dhambi, hatushikiliwa tena na nguvu zake katika maisha yetu.
Je, ni nini maana ya kujihesabu? (Warumi 6:11). Ni neno linalohusika na utunzaji wa mahesabu. Inamaanisha ni kujihesabu kwa kile ambacho ndicho. Neno la Kiyunani linatumika mara 11 kwenye Agano Jipya, ingawa katika vifungu tofauti imetafsiriwa katika maneno tofauti. “Kwa hapa inamaanisha kwamba ni “kutengwa kwa imani ya uhuru wa kutoka kwenye dhambi na muungano na Mungu uliotolewa katika upatanisho na kufufuka kwa Kristo.”[2]. Kitenzi kinaonesha kuwa tunapaswa kuamini kile ambacho tayari kimeshakuwa kweli:tumekufa katika kufanya dhambi.
Je, inanipasa kufanya nini ili kuonesha kweli kwamba nimekufa kufanya dhambi na kuwa ninaishi katika Kristo Yesu? Kwa imani ninapokea Neno la Mungu kama Ukweli kwa ajili ya moyo wangu. Natangaza juu ya mamlaka ya neno la Mungu lililovuviwa na lisilo na makosa kwamba nimewekwa huru kutokana na dhambi zote na kufanywa kuwa hai kabisa kwa Mungu katika Kristo Yesu aliye Bwana wangu.
Kama mtumwa wa upendo na hiari wa Yesu Kristo, kwa hiari yangu mwenyewe ninaachana na tabia hizo na matendo yote ambayo yalikuwa ni sifa bainifu za matendo ya zamani. Kujisalimisha kikamilifu kwa Yesu ni furaha! Na kwa matokeo ya uhusiano wangu na Kristo, ninayo maisha ya milele.
Hitimisho
Tumeshaona kwamba ni heshima yetu iliyonunuliwa kwa damu kuwa na uhuru kutokana na nguvu ya kutawaliwa na dhambi. Lakini zaidi y hapo, ni agizo la Mungu kwamba tuwe washindi.
[3]Pengine huko nyuma hujaweza kutambua huu ukweli. Mungu amekuokoa wewe na unatembea katika upya wa maisha; lakini unakuta kwamba dhambi bado inazidi kujitokeza katika maisha yako. Hupendi iwe hivyo! Lakini ndani yako kuna kitu ambacho kinataka kufanya vitu kivyake. Kama hivi ndivyo, fuata agizo la Paulo la kujihesabu mwenyewe kuwa umekufa kabisa kwa dhambi (6:11) na kujitoa mwenyewe kwa Mungu (6:13).
Mkabidhi yeye udhibiti wote! Kama utafanya hivyo, anaahidi kukuwezeshakuishi maisha huru kutoka nguvu ya udhibiti wa dhambi. Amini kile Mungu anachosema na udai kwa imani uhuru wako wa kutoka katika dhambi.
► Je, inamaanisha nini kuungana na Kristo? Je, ni nini utegemee kwenye maisha yako kwa sababu umeunganika na Kristo?
“Tunaposoma Warumi 6-8 tutagundua kwmaba hali ya kuishji kawaida maisha ya kikristo yana sehemu nne. Nayo ni
(1) kujua, (2) kujihesabu,
(3) kujiweka nafsi zetu kwa Mungu, na (4) kutembea katika roho , na yamepangwa katika utaratibu huo.”
- Watchman Nee, The Normal Christian Life
Jinsi ya Kuishi Maisha ya Ushindi
Je, ulishawahi kujiuliza kama kweli inawezekana kuishi kwa ushindi kabisa dhidi ya dhambi? Mungu ameahidi kutuwezesha neema ambayo ni zaidi ya fidia kwa madhaifu yetu katika majaribu:
Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili (1 Wakorintho 10:13).
Aya hii inatuelezea mambo mengi muhimu:
1. Kila jaribu ni jambo la kawaida kwa mwanadamu. Linatokea kwa sababu ya ubinadamu wetu na linalenga kwenye madhaifu kadhaa ya kibinadamu. Hii ina maana kwamba mapambano yako siyo ya kipekee kwako.
2. Mungu anajua mipaka yetu. Anajua ni kwa jinsi tunaweza kuwa na uvumilivu. Hatujui kwa uhakika ni kwa jinsi tunaweza tukavumilia, lakini yeye anajua.
3. Mungu huweka mipaka ya majaribu yanayokuja kwetu kwa sababu anataka tuishi kwa ushindi. Watu wengine wanadhania kwamba majaribu mara nyingi yatakuwa juu ya uwezo wetu kwa sababu sisi ni wanadamu. Wanadhani kwamba haiwezekani kuwa na ushindi wa kudumu, lakini kwa mujibu wa aya hii sivyo ilivyo.
4. Mungu hutoa kile ambacho tunahitaji kwa ajili ya kuishi kwa ushindi. Hufanya njia ya kutokea.
Kwa hiyo hitimisho ambalo tunaweza kulipata kutoka katika aya hii ni kwamba Mungu anatukusudia tuishi maisha ya uhuru. Neema kwa ajili ya maisha ya ushindi hutolewa kwa kuitikia imani.
Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu (1 Yohane 5:4).
Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao (Yakobo 1:12).
Kama tutaelewa imetokeaje kwamba waamini wameshindwa na majaribu, inawezekana tukaelewa pia na jinsi ya kuzuia. Mtu anayeangukia kwenye majaribu kwa kawaida amejiruhusu yeye mwenyewe kupitia katika mchakato fulani.
Mchakato huo umeelezwa katika Yakobo 1:14-15: “Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti…”
John Wesley aliona kwamba hatua za kutenda dhambi kwa hiari kwa kawaida hufanyika kama ifuatavyo:
1. Jaribu hujitokeza (kutoka katika dunia, mwili, au Shetani).
2. Roho Mtakatifu humonya mtu aliyeamini awe mwangalifu.
3. Mtu huweka usikivu wake kwenye jaribu na mvuto wake huongezeka. (Kwenye mchakato huu, hapa ndipo mtu anapofanya kosa lake la kwanza.)
4. Roho Mtakatifu huhuzunishwa, imani ya mtu hufifishwa, na upendo wake kwa Mungu unakuwa baridi.
5. Roho Mtakatifu hukemea na kusahihisha kwa uchungu.
6. Mtu hugeuka katika kusikiliza sauti yenye maumivu ya Roho Mtakatifu na kuanza kusikiliza sauti ya kuvutia kutoka kwa mjaribu.
7. Matamanio ya uovu huanza na kuujaza moyo wake; imani na upendo hutoweka; na yuko tayari kufanya dhambi ya wazi.
Hatupaswi tudhanie kwamba uzoefu wa kila mtu kwenye kutenda dhambi siku zote utakuwa unafanana na mpangilio huu. Mara nyingine watu hujitoa kwa ghafla kutenda dhambi hata bila kufuata mchakato wowote.
Kwa kuwa jaribu huongezeka nguvu yake wakati tukiwa tunashikilia usikivu wetu, mtu aliyeamini ambaye yuko makini katika kuimarisha ushindi wake dhidi ya dhambi ni lazima auimarishe moyo wake ili aweze kulikataa jaribu mara moja. Mtu anayetambua kwamba jaribu linampeleka kwenye kufanya dhambi lakini akasita kulizuia linamweka kwenye hatari kubwa zaidi. Kwa kusitasita, anajidhihirisha kwamba moyo wake haujaamua kwa ukamilifu kumpendeza Mungu.
Jaribu ni changamoto kwa imani yetu, kwa kuwa linatupa sisi nafasi ya kuwa na shaka kwamba utii kwa Mungu ndiyo njia nzuri zaidi kwa wakati huo.
► Kama inaonekana kwamba mtu aliyeamini anashindwa kuishi kwa ushindi dhidi ya dhambi, je, kuna sababu gani katika hilo?
Inawezekana ikawa ni kwa sababu mojawapo ya matatizo yafuatayo:
1. Haoni kwamba Mungu anahitaji utii.
2. Haoni au haamini ahadi ya Mungu ya neema inayowezesha.
3. Hategemei neema ya Mungu inayowezesha badala yake anategemea nguvu zake mwenyewe.
4. Anamtumikia Mungu huku akiwa na chaguo la aina ya utii atakaouonesha badala ya utii kamili, na ambao hauna masharti.
5. Hajatafuta kwa neema kuwa na lengo moja la kufanya mapenzi ya Mungu (Wafilipi 3:13-15).
6. Hajadumisha nidhamu ya kiroho ambayo itampa nguvu ya imani ya kujenga uhusiano na Mungu.
7. Hatimizi uwajibikaji wake wa kiroho kwenye kanisa lake la mahali pamoja.
8. Mara kwa mara hatafakari neno la Mungu.
9. Haja zoeza hisia zake katika kusikia sauti ya Roho Mtakatifu katika maisha yake.
Watu watatu waliomba kazi ya udereva wa kumwendesha mwajiri wao. Yule wa kwanza, akitaka kumvutia mwajiri wake mtarajiwa, akasema, “Mimi ni dereva mwenye uwezo wa hali ya juu sana kiasi kwamba hata nikaendesha gari kwa mwendo wa kasi futi chache tu kutoka kwenye mteremko mkali wa mlima uliochongoka hutahitaji kuwa na wasiwasi.” Yule wa pili naye hakutaka kupitwa na mwenzake, akasema, “Mimi ninaweza nikaendesha kwa mwendo wa kasi inchi chache tu kutoka kwenye mteremko mkali wa mlima uliochongoka bila kupita juu yake na hutahitaji kuwa na wasiwasi.” Yule mwombaji wa tatu akasita, kisha akamwambia yule mwajiri, “mimi sitadiriki kuhatarisha maisha yako kwa kupita karibu na huo mteremko mkali wa mlima uliochongoka.” Unadhani ni yupi katika hawa waombaji watatu aliyepata ajira?
Hatupaswi tuangalie ni kwa karibu kiasi gani tunaweza kufika kwenye jaribu. Mungu anataka atupe sisi miongozo ambayo itatuongoza kwenye maeneo ya madhaifu yetu.Tunapaswa tujifunze ni mambo gani yenye madhara, kama vile baadhi ya burudani mbalimbali, na kukaa mbali na mambo hayo.
Kama mtu aliyeamini hajadumisha uhusiano wake na Mungu, anapaswa kwa haraka atubu na kurejeshwa tena kwa Mungu kupitia kwa wakili wetu Yesu Kristo (1 Yohane 2:1-2). Hapaswi angojee muda wowote ujao ambao anauona kwamba utakuwa ni mzuri kwake. Kama anataka kurejeshwa, Roho Mtakatifu atampa hiyo nia na kumrudisha alikotoka kwenye uhusiano wake na Mungu. Kama toba yake ni ya kweli, anaweza akarejeshwa mara moja.
Mungu tayari alishafanya uwekezaji mkubwa kwa ajili ya wokovu wetu, katika dhabihu ya Yesu. Hayuko tayari kuachilia huo uwekezaji alioufanya upotee bure kwa kushindwa kutupa sisi neema tunayoihitaji ili tuendelee mbele.
Kweli Tano za Kujua na Kuzidai
Ushindi dhidi ya matendo ya dhambi ni zoezi la kawaida la Mkristo kwa sababu amewekwa huru kutoka katika utumwa wa dhambi kwa kifo, kuzikwa, na kufufuka kwa Yesu.[1] Kuendelea kukaa kwenye dhambi kunatokana na kupuuzia neema ya Mungu inayookoa, kushindwa kukaa kwenye muunganiko na Yesu, kushindwa kuendelea kujihesabia binafsi kwamba umekufa kwa dhambi na unaishi kwa Mungu na kushindwa kuwakilisha kikamilifu na kwa uamuzi wa dhati mwili wa mtu kwa Mungu kama chombo cha haki.
Kila mwamini wa kweli anatamani kuwa na uzoefu wa ushindi dhidi ya dhambi. Hii ni kwa sababu ya gharama kubwa Yesu aliyolipa ili kutukomboa kutokana na dhambi. Hii ni kwa sababu ya asili ya uharibifu ya dhambi. Jibu la Paulo kwa wale ambao wangehoji kwamba “Je, kwa kuwa neema inakua kwa ajili ya dhambi, kwa nini tusiendelee kutenda dhambi?" kunakoonekana kuwa na nguvu sana. “Hasha!” anasema (Warumi 6:1-2). Kwa mtu kuwa na tabia ya kizembe kuelekea ugonjwa wa dhambi kisa tu kwa sababu Mungu ameleta tiba kwa ajili ya hilo itakuwa ni sawasawa tu na kuwa mzembe kwenye ugonjwa wa UKIMWI na Kansa kisa tu kwa sababu tiba imegundulika. Tiba haiwezi kumsaidia mtu wakati wa maumivu au ugonjwa. Wala haiwezi kumwepusha mtu na makovu. Hakuna mtu mwenye akili timamu atakayeweza kusema, “Acha tuugue ili kwamba tuweze kupata tiba.” Hakuna mtu aliyeona ubaya wa dhambi, makosa ya dhambi kwa Mungu mtakatifu, na gharama ya kutisha iliyolipwa kwa ajili ya kuondoa dhambi atakayesema, “Tutende dhambi kwa kuwa maana neema itazifunika zote!”
Uzoefu wa Mkristo wa uhuru kutokana na dhambi unategemea juu ya ufahamu wake (Warumi 6:3, 6, 9) na matumizi ya hizi kweli:
(1) Kama mwenye dhambi mimi nilikufa
“Utu wa kale” ambao mtu mtenda dhambi wa zamani kama tulivyokuwa, kiroho ulikufa pamoja na Kristo pale juu ya msalaba na alizikwa pamoja naye kwenye kaburi lake. Kwa kuwa mtu aliyekufa hawezi tena kutumika kama mtumwa, ubwana wa dhambi juu yetu umevunjika. Kifo hiki tayari kilishatokea. Kifo cha maisha yetu ya dhambi ya zamani kilifanyika mara tu tulipoamini katika kifo cha Kristo kwa ajili yetu, tulipotubu kwa ajili ya dhambi zetu, na tukapokea zawadi yake ya uzima wa milele.
Angalia maneno haya kutoka kitabu cha Warumi 6:
“…Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?” (6:2).
“…Sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake” (6:3).
“Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake…” (6:4).
“Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake...” (6:5).
“Mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena” (6:6).
“Kwa kuwa yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi” (6:7).
Tatizo lililoko kwa waamini wengi wakati wa sasa ni kwamba wanaishi chini ya uwezo wao. Waamini wengi wamejiweka kwenye hali ya kukubali kushindwa kama jambo la kawaida. Wanafikiri kwamba maisha ya ushindi kwa Mkristo ni jambo lisilowezekana na kwamba ni na kwamba wanategemea kuendelea kuishi katika dhambi. Waamini wengine wanafikiri kuwa hakuna kuvumilia kumvumilia anayeshindwa mtu lazima awe mkamilifu. Mafundisho haya pia ni uharibifu kwa imani na yameelekeza wengi aidha kwenye kukata tamaa au kuwa wanafiki. Paulo anaweka bayana kwamba ushindi ni wetu kupitia ushirikishwaji wa ushindi wa Kristo pale msalabani.
(2) Mungu amenifufua pamoja na Yesui li kuwa mtu mpya
Yesu alizishinda dhambi zote kupitia kufufuka kwake. Ni maisha ya ufufuko ambayo tumekuja kushirikishana kwa imani. Kwa imani, dhambi haina uwezo tena wa kutuweka chini, kutudhalilisha, kutujeruhi au kutuua sisi. Kiroho tulifufuliwa pamoja na Kristo kwenye maisha mapya ya ushindi.
“…Kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima” (6:4).
“…Kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake” (6:5).
“Tukijua ya kuwa Kristo akiisha kufufuka katika wafu hafi tena, wala mauti haimtawali tena” (6:9).
“Maana kwa kule kufa kwake, aliifia dhambi mara moja tu; lakini kwa kule kuishi kwake, amwishia Mungu” (6:10).
“Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu” (6:11).
“Jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa...” (6:13).
(3) Nimeunganishwa kiroho na Yesu.
Siyo tu kwamba maisha yangu ya zamani yamesulubiwa pamoja naye, na siyo tu kwamba nimepokea maisha mapya kama yake; bali ninakaa ndani yake, na yeye ndani yangu! (Ona pia Wagalatia 2:20 na Yohane 14-16.) Hii ni ahadi iliyoahidiwa na Yesu kwa kila Mwanafunzi: kwamba Mungu amechchagua kukaa ndani ya waamini kwa njia ya Roho Mtakatifu. Muungano huu pamoja na kukaa ndani yetu ndicho kinachosababisha ushindi dhidi ya dhambi na kufanya iwezekane kuishi maisha matakatifu. Hii ndiyo inayofanya iwezekane kwa waamini kupokea kuishi kwa usafi, upendo, wenye huruma, wapole, wenye kusamehe na maisha matakatifu kwa ajili ya Yesu.
“Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake” (6:5).
“…Utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye...” (6:6).
“Lakini tukiwa tulikufa pamoja na Kristo, twaamini ya kuwa tutaishi pamoja naye” (6:8).
Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kuhusu muungano huu katika Yohane 15. Fundisho la imani kuhusiana na muungano wa kiroho pamoja na Kristo ni muhimu kwa ajili ya mafanikio yetu katika maisha ya Kikristo!
(4) Ni lazima nimiliki kwa imani uhuru na ushindi Mungu aliotupa sisi.
Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu (6:11).
Kujihesabia ni kuhesabu kama jambo hili ni kweli ili kwamba uweze kupata uzoefu katika maisha yako mwenyewe.
Hapa kuna kielelezo kutoka katika Agano la Kale ambacho kinaweza kuwa cha msaada. Tunakumbuka kwamba Mungu hakuwa tu amewaahidi Waisraeli ardhi yaani nchi ya Ahadi, bali pia alikuwa amewapa hiyo nchi muda mrefu hata kabla hawajaimiliki kiukweli. Kwa miaka arobaini walizunguka jangwani, wakiishi chini ya kiwango cha uwezo wao, kwa sababu walijiingiza katika hofu na walishindwa kumwamini Mungu. Lakini Mungu aliwapenda na akawaongoza kwenda kwenye urithi wao.
Katika Yoshua 1:3 panasomeka, “Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa.” Kwenye aya nyingine za baadaye Mungu anaagiza, “Piteni katikati ya matuo, mkawaamuru hao watu, mkisema, ‘Fanyeni tayari vyakula; kwa maana baada ya siku tatu mtavuka mto huu wa Yordani, ili kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wenu, mpate kuimiliki’” (Yoshua 1:11).
Watu wa Mungu wanatakiwa, kwa imani, wamiliki nchi ambayo Mungu amewapa. Wakati ushindi juu ya wakazi wa kimwili wa Kaanani ulipotolewa, na kwa kila hali ikawa umekamilika, Waisraeli walikuwa wauzoee ushindi huu kupitia imani ya utii. Waamini wa Agano Jipya hushinda kwa njia hiyo hiyo; kwa kujihesabia, kwa imani, kwa ushindi wa Yesu Kristo alioufanya kwa ajili yetu na kumiliki ahadi mbalimbali.
(5) Ni lazima niutoe mwili wangu kwa Mungu.
Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake. Wala msiendelee kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi; bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki (Warumi 6:12-13).
► Wanafunzi mbalimbali watapaswa watoe ufafanuzi kuhusu umuhimu wa kweli tano zilizoko katika kifungu kilichotangulia.
Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? (Warumi 8:32).
Yeye awezaye kuwalinda ninyi msijikwae, na kuwasimamisha mbele ya utukufu wake bila mawaa katika furaha kuu; Yeye aliye Mungu pekee, Mwokozi wetu kwa Yesu Kristo Bwana wetu; utukufu una yeye, na ukuu, na uwezo, na nguvu, tangu milele, na sasa, na hata milele. Amina (Yuda 24-25).
Maswali ya Mapitio Somo la 6
(1) Je, kwa nini ni muhimu kuelewa dhambi ni nini?
(2) Je, maana ya dhambi ya kukusudia ni nini?
(3) Ni dhana gani potofu ambayo Paulo anaijibu katika Warumi 6?
(4) Je, kuifia dhambi ina maana gani?
(5) Je, ina maana gani kuwa chini ya neema?
(6) Je, kuwa chini ya sheria ina maana gani?
(7) Je, kwa nini ni haiwezekani kumtumikia Mungu na dhambi?
(8) Je, msemo wa utu wa kale maana yake ni nini?
Kazi ya kufanya Somo la 6
(1) Andika ukurasa mmoja ukielezea ni ushindi gani unaowezekana dhidi ya dhambi kwa mtu aliyeamini. Husisha pamoja na ufafanuzi wa dhambi ya hiari au kujitakia, na elezea kwa nini ufafanuzi wa dhambi ni muhimu. Jibu upinzani wa watu wanaotoa kuhusu uwezekano wa ushindi dhidi ya dhambi.
(2) Unahitajika kumalizia uwakilishaji wa mahubiri au masomo yako matatu.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.