Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu 5, kifungu cha 2-3
Warumi 10 ni kilele cha kitabu cha Warumi. Mtume tayari alishaeleza kwamba wokovu ni kwa neema kwa njia ya imani na kwamba kila mtu katika ulimwengu huu anauhitaji. Kwa kuwa imani ni ya lazima, ujumbe wa injili ni muhimu: Watu wanahitaji kusikia ujumbe ili kwamba waweze kuuamini. Sura hii ni ya muhimu katika kusudi la kitabu kwa sababu kitabu chote kinatoa msingi wa kazi ya umishenari.
Warumi 11 inahusika na mahusiano kati ya Waisraeli na Kanisa. Wayahudi wengi waliikataa injili. Paulo alielezea kwamba mpango wa Mungu ulikuwa ni dunia yote pamoja na Wayahudi waweze kuokolewa. Waisraeli kwa ujumla wao kuna siku moja watakayomkubali Kristo.
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu 5, kifungu cha 2
Jambo Kuu katika Warumi 10
Haki ni lazima ipatikane kwa imani, na umuhimuwa imani uhafanya ujube wa injili uwe na umuhimu wa haraka.
Muhtasari wa Warumi Sura ya 10
Ni kosa kujaribu kuhesabiwa haki kupitia kujihesabia haki binafsi. Haki ambayo Mungu huikubali kutoka kwa mwanadamu, yeye kwanza anampa mwanadamu kutokana na mwitikio wake wa imani. Ujumbe wa injili unatoa nafasi kwa ajili ya imani.
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 10 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo ya Aya-kwa-Aya
(10:1-5) Wayahudi bado wanahitajika waokoke kwa sababu hawakuelewa haki waliyoihitaji ni kitu gani. Walijaribu kujihesabia haki wenyewe kwa kuanzisha kumbukumbu mahususi za haki binafsi, bila kutambua kwamba jambo hilo lilikuwa haliwezekani. Haki ambayo Mungu anaikubali ni ile ambayo yeye anaifanyia kazi ndani ya mtu kwa mwitikio wa imani.
Kusudi la sheria ni kutuleta sisi kwa Kristo kwa kulaani dhambi na kuonesha hitaji kwa ajili ya Mkombozi. Wakati mtu anapokuja kwa Kristo, sheria haiwi tena kwamba ndio msingi wa kukubalika kwake na Mungu, hivyo Kristo huwa ndio mwisho wa hiyo sheria (10:4). Hiyo haimaanishi kwamba sheria haituoneshi tena njia ya kumtii Mungu, lakini kukubalika kwetu na Mungu hakutegemei sisi kuwa na kumbukumbu ndefu ya utii uliokamilika na wa muda mrefu.
Nadharia kwamba watu walioishi kabla ya Kristo kuja waliokolewa kwa matendo yao moja kwa moja inakataliwa na kifungu hiki. Paulo anaelezea waziwazi kwamba watu wote waliojaribu kutengeneza haki yao wenyewe kwa njia ya matendo walikuwa wamepotoshwa na kupotea. Wangepaswa waamini ukweli wa injili ambao Paulo aliunukuu kwenye 10:6-8 kutoka katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati.[1]
(10:6-11) Hii ni nukuu ya Kumbukumbu la Torati 30:11-14. Musa aliwaambia Waisraeli kwamba kuzishika amri za Mungu na maagizo yake hakutegemei kiwango fulani cha ushujaa au nguvu za kibinadamu zisizo za kawaida, kama vile kupaa mbinguni au kuvuka bahari. Badala yake itakamilishwa ndani yao na Mungu kupitia katika imani yao.Paulo alitohoa taarifa hii akirejelea kwenye matendo ya ajabu ya kupaa kwenda mbinguni au kushuka duniani na akaonesha kwamba Kristo alishatimiza mambo yote yaliyokuwa muhimu.
[2]Wokovu kwa njia ya neema ni karibu mno kiasi kwamba uko ndani ya mioyo na midomo yetu kwa sababu tunaupokea kwa imani (mioyoni mwetu) na kwa kuukiri (kwa vinywa vyetu).
(10:12-13) Hapa kuna msisitizo mwingine kwamba njia hiyo hiyo ya wokovu inapatikana kwa kila mtu. Yesu ni Bwana juu ya kila kitu, na mtu yeyote aliyeko mahali popote katika dunia hii anaweza akamwita.
(10:14-15, 17) Huu ni wito kwa ajili ya kazi ya umishenari. Ujumbe wa mishenari ni wa haraka - Kwa kuwa watu wanaokoka kwa imani, wanahitaji kusikia ujumbe ambao utawapeleka katika kuamini. Aya hizi ni za umuhimu wa kina kwa kusudi la kitabu hiki.
Paulo anaonesha shauku kubwa kwa ajili ya kazi ya mmishenari na anaelezea mkasa kwa wale ambao watakuwa hawajaisikia injili. Wanaweza wakaokoka kwa kuamini, lakini wataaminije wasiposikia, na watasikiaje kama hakutapelekwa mmishenari?
► Paulo alizungumzia hitaji la kutuma wamisionari, yaani kusaidia katika kuwawezesha na kuwapa misaada inayotakiwa. Wewe utakuwa unafanya nini kwa ajili ya kumsaidia kupeleka injili kwa watu ambao hawako karibu na wewe?
(10:16, 18-21) Kuingizwa kwenye wito wa umisheni ni ukumbusho kwamba siyo watu wote watakaokubali mwitikio huo. Watu hawaokoki kwa taarifa ya injili peke yake. Wamataifa walikuwa na taarifa ya Ufunuo wa Ujumla (uliojadliwa katika 1:18-20), lakini hilo halikuweza kuwa sababu ya wao kuokoka kwani walilikataa (10:18 ni nukuu kutoka Zaburi 19:4). Waisraeli walikuwa na ufunuo wa zaidi, hata hivyo, hawakuokoka kisa tu kwa kuwa walikuwa na ufunuo huo. Isaya alikuwa ametabiri kuhusu Waisraeli kumkataa Masihi (Isaya 53:1, 3).
Mtume anajibu hizi pingamizi. Kwanza, kuhusu Wamataifa, mtu anaweza akasema, “Lakini kweli hawajui?” Paulo anajibu, “Ndiyo, ufahamu wa Mungu uko kila mahali,” kama alivyoeleza katika 1:20. Kisha, mpinzani anauliza kuhusu Wayahudi: “Je, Israeli haikujua?” Paulo anajibu kwamba Mungu anaendelea kuwafikia Waisraeli, lakini, walikataa kutii. Mpinzani ana mashaka na ufanisi wa ujumbe wa injili kwa sababu wengi waliusikia na hawakuokoka.
Paulo alielezea kwamba Waisraeli wengi hawakuitikia kwa imani.[3] Watu hawaokoki kwa ujumbe hadi wawe wameitikia.
Kuhubiri hakuwezi kumfanya mtu aliyekataa aweze kuokoka – Neema ya Mungu si kitu ambacho hatuwezi kupinga. Hata hivyo, inatoa nafasi ya wokovu. Ingawaje kila mtu anajua chochote kuhusiana na Mungu, injili inakuja na nuru kubwa zaidi na nguvu kubwa ya kuona hatia kutoka kwa Roho Mtakatifu.
[2]“Barua za Paulo zinaonesha kuwa uinjilisti wake ulikuwa na misukumo miwili: hali ya uwajibikaji inayokuja kutokana na yale ambayo Mungu alimfanyia na kumpa jukumu la kuwafanyia wengine, na hamu kwamba Mungu atatukuzwa na watu wengi kadiri inavyowezekana.Tunapaswa kumwiga Paulo kwa kutoa neema ya Mungu katika injili kama alivyofanya.”
- Douglas J. Moo, Romans
[3]Ona sehemu iliyoko katika somo la 4 yenye kichwa cha habari "Neema katika Agano la Kale."
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu 5, kifungu cha 3
Jambo Kuu katika Warumi sura ya 11
Hakuna mtu yeyote anayeweza kuokoka bila ya kukubaliana na vigezo vya Mungu vya wokovu.
Muhtasari wa Warumi 11
Waisraeli kwa ujumla hawakuokoka kwa sababu walikataa kuokolewa katika njia ya Mungu. Wengi wa Wamataifa waliokoka, lakini yeyote aliyeanguka kutoka katika imani aliupoteza wokovu wake. Wayahudi wanaweza wakaokoka kama wataamua kuchagua hivyo, na Israeli kwa ujumla wake kuna siku moja wataikubali injili. Mungu atatimiza ahadi zake alizozitoa kwa mababu zao.
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 11:1-15 kwa ajili ya kikundi.
Maelezo ya Aya-kwa-Aya
(11:1) Swali ni kwamba, “Je, Mungu amewakataa Wayahudi?” Paulo anajibu, “Hapana, Na mimi pia ni Myahudi.” Baadhi ya Wayahudi waliokoka.
(11:2-5) Wale amabo Mungu aliwajua hawakataliwi. Bila shaka, Mungu alimjua kila mtu kwa mantiki kwamba yeye ni mjuzi wa mambo yote, lakini wale aliowajua kwa mantiki ya aya hii haiwezekani ikawa ni kila mtu kwa sababu aya inazungumzia kuhusu watu maalumu wa Israeli. Aya inahusiana na wale ambao Mungu anajua watakuwa na mwitikio wa neema yake.[1] Paulo anatoa mfano wa watu ambao Mungu aliwajua katika mantiki hii na wakakubalika – watu 7,000 ambao hawakumwinamia Baali.
Masalia ambao wamechaguliwa na Mungu (11:5) hawakuchaguliwa kiholela au bila ya utaratibu maalumu. Walikuwa na watu ambao Mungu aliwajua kwamba watamwamini yeye.
(11:6) Matendo na neema siku zote huenda kwa pamoja katika maisha ya Mkristo, lakini vyote vinatofautiana katika msingi wa wokovu. Huwezi kuvichanganya pamoja kwa msingi wa kukubaliwa na Mungu, kama dini za uongo zinavyofundisha.
(11:7-10) 11:8, ambayo ni nukuu kutoka Isaya 29:10, inaonesha kuwa watu kutokuwa waaminifu kuliwafanya wawe vipofu kiroho. Mioyo yao ikawa migumu kwa kuwa waliendelea kuikataa kweli. Isaya 6:9-10 vile vile inasema kwamba watu huwa vipofu wanapoendelea kusikia na kukataa rehema inayooneshwa. Mistari hii katika Warumi haina maana kuwa Mungu alikataa kuonesha rehema kwa baadhi ya watu. Laana ya Daudi (Zab 69:22, 23), ambayo Paulo ananukuu katika Warumi 11:9-10, haikuwa ni kutubu ambayo watu wangekataliwa, lakini watu waovu wangehukumiwa.
(11:11) Je, Mungu amewaruhusu kuanguka kiasi cha kutokuwa na matumaini tena? Hapana. Suala la Waisraeli kumkataa Kristo lilisababisha kusulubiwa kwake, ambao ulikuwa ni mpango wa Mungu wa wokovu. Katika mantiki hii, kukataa kwao kulisababisha kukubaliwa kwa Wamataifa. Wakati Wayahudi watakapowaona Wamataifa wakiokoka, wataelewa kwamba hata wao wanaweza wakaokoka kwa njia hiyo.
(11:12-15) Wamataifa watafaidika zaidi endapo Waisraeli watamrudia Mungu. Siyo muhimu kwa Mungu kuchagua kati ya Wayahudi na Wamataifa. Anataka awaokoe wote.
► Baadhi ya wanateolojia wanaamini kwamba kwa kuwa Mungu huchagua kutokuwaokoa baadhi ya watu, ameiondoa neema yake kwao, jambo linalofanya wasiwe na uwezo wa kuokoka. Je, utajibuje wazo hilo kutoka katika 11:12-15?
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 11:16-24 kwa ajili ya kikundi.
(11:16-24) Aya hizi zinatumia mfano wa kuchukua tawi la mti na kulipandikiza katika mti mwingine. Waisraeli walikuwa kama ni matawi yaliyokatwa kutoka kwenye mti wa Mungu, na Wamataifa kama matawi yaliyoongezwa kwenye mti huo, ambayo hayakuwa sehemu ya mti hapo awali. Wayahudi walikatwa kwa sababu ya kutoamini kwao. Mtu yeyote aliyeletwa katika mti huo atakatiliwa mbali pia kama hataendelea kuwa ndani ya imani katika mti huyo. Wale ambao walikataliwa mbali wanaweza pia wakarejeshwa tena.
Paulo hakusema kwamba Mungu huamua ni nani awe kwenye mti na kwamba uamuzi wake haubadiliki. Alisema kwamba Mungu huwaondoa wale watu ambao hawajaamini, lakini atawaingiza tena kama wakiamini. Wamataifa wanaoamini wanaingia, lakini watakatiliwa mbali endapo wataangukia kwenye kutoamini. Mungu huitikia kwenye chaguo la wanadamu wenyewe.
► Kutokana na aya hizi, jinsi gani ungeweza kuelezea mfano wa matawi yanayoongezwa au kuondolewa?
Ni muhimu kufahamu ni kitu gani Biblia inafundisha kuhusu usalama wa mtu aliyeamini. Biblia ina maonyo mengi mazito kwa ajili ya watu walioamini.
Katika Yohane 15:2-10 ni mfano uliokuwa maarufu sana wa mzabibu na matawi. Mfano huu unajibu baadhi ya maswali mengi.
Je, tunakaaje ndani ya Kristo? "Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu” (15:10). Kuacha kukaa ndani ya Kristo inamaanisha kwamba ni mtu aliacha kumtii yeye. Kisha, ni nini kinachotokea baadaye?
“Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea” (15:6). Kama mtu ataacha kutii na hapo akaacha kukaa ndani ya Kristo, atakataliwa. Mfano wa matawi yakianguka kutoka kwenye mzabibu kisha yakakusanywa na kutupwa motoni inaonyesha kukataliwa kabisa kwa kiasi ambacho hatuwezi hata kufikiria.
“Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu (15:4) “Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa” (15:2). Kuzaa matunda ni kuishi maisha yaliyobadilishwa, yaliyobarikiwa, na kuongozwa na neema ya Mungu. Kama hatutakaa ndani ya Kristo kwa njia ya utiifu, hatuwezi kuzaa matunda. ikiwa na maana ya kuishi maisha yaliyobadilishwa, yaliyobarikiwa, na yanayoongozwa na neema ya Mungu. Mtu asiyezaa matunda atakataliwa
Biblia haijatuambia mahali popote kwamba tutaendelea kuwa na wokovu bila kujali ni jambo gani tumefanya. Neema endelevu kwa kuishi kikristo inakuwepo kupitia uhusiano wetu na Mungu kwa njia ya Kristo. Kristo ni kama mzabibu ambao ni lazima tuendeleze maisha kutokea hapo. Mfano wa mzabibu unaonyesha kwamba kipawa cha wokovu kinapatikana kwa njia ya uhusiano. Kutengwa kutoka kwa Kristo ni kutengwa kutoka kwenye wokovu. Tunadumisha huu uhusiano wa wokovu wetu kwa kumtii Mungu.
Glopu ya umeme na umeme wenyewe inaweza kwa mfano wa kisasa. Glopu ina mwanga wakati umeme unakuwa unatiririka ndani yake. Glopu haiwezi ikawaka kama itakuwa imezimwa kutoka kwenye chanzo chake cha kupata umeme. Vivyo hivyo, tunao uzima wa milele kwa kuwa tuna uhusiano wetu na Kristo. Uhai wake unatiririka ndani yetu. Hatuwezi kuuendeleza na kuudumisha uhai huo wa maisha kama tutajitenganisha kutoka kwake.
Maandiko yanatuonya kwamba mtu aliyeokoka anaweza akapoteza wokovu wake kama mwishoni atashindwa katika dhambi. “Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima (Ufunuo 3:5). Hawa walikuwa ni watu waliokuwa wameokoka, lakini bado wokovu wao utapotea kama watakuwa wameshindwa katika dhambi.
Wakati fulani, Paulo alikuwa na mashaka kwamba watu wake walioamini na kuokoka katika Thesalonike watakuwa wameachana na imani. Alisema kwamba kama hali hiyo itakuwa imetokea, kazi yao ya uinjilisti itakuwa haina faida (1 Wathesalonike 3:5). Hii inaonesha kwamba kuna uwezekano wa mtu aliyeamini kuanguka kabisa kutoka katika imani yake kiasi kwamba kuokoka kwake kutokea mwanzo hakuna faida tena.
Katika 2 Petro 2:18-21 tunaona kwamba kuna waalimu wa uongo ambao huwadanganya watu walioamini, yaani “wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo.” Watu hawa waliokuwa wameamini walikuwa wameijua njia ya haki lakini wakaiacha. Andiko hili linasema kwamba ingekuwa afadhali wasingejua njia kuliko kurudi kwenye maisha ya dhambi. Hii inaonyesha kwamba inawezekana mtu kupoteza wokovu wake kwa kurudi tena dhambini. Kama ingekuwa haiwezekani kwa mtu aliyeamini kuupoteza wokovu wake, mtu hawezi kamwe kuwa mbaya zaidi kuliko kabla ya kuokolewa.
Mungu anataka watu walioamini wajisikie wako salama, lakini siyo kuwekeza hisia zao kwenye uhakika potofu au wa kudanganyika ambao unawaweka katika hali halisi ya hatari ya kiroho. Hatupaswi kuwaahidi watu walioamini kitu ambacho Mungu hajawahi kuwaahidi. Mungu hajawahi kutoa ahadi kwamba tutakuwa salama endapo tutapoteza wokovu wetu kutokana na lolote lile tutakalolitenda.
Mungu anaahidi kuwa pamoja nasi, kutuongoza, na kutupa uwezo wa kuishi kwa ushindi dhidi ya dhambi. Anaahidi kwamba tutapokea maisha ya kiroho kutokana na uhusiano wetu pamoja naye. Mtu aliyaeamini anaweza kuishi bila hofu ndani ya ahadi ya Mungu ya neema endelevu ambayo mwamini hupokea akiwa kwenye mahusiano na Mungu.
Kifungu cha kujifunza – Warumi Sehemu ya 5, kifungu cha 3
Mwendelezo wa maelezo ya Aya-kwa-Aya
(11:25-29) Israeli kama taifa (Waisraeli wote) wataokoka. Hii haimaanishi kwamba kila Myahudi binafsi ataokoka, lakini kwa muda wa mbele baadaye masalia wa imani katika taifa hilo watamgeukia Mungu. Ukamilifu wa watu Wamataifa umeelezwa katika Luka 21:24. (Taarifa nyingine kuhusiana na wokovu kwa Waisraeli kama taifa unapatikana katika Isaya 2:2-5, Isaya 60:1-22; Zekaria 12:7-13:9).
(11:30-31) Ona maelezo katika 11:11.
(11:32) Mungu amewaweka katika kundi moja wote kama watu wasioamini walioko katika hali moja. Mungu amehukumu wote na kutamka hukumu juu yao, ili wawe ni stahiki sawa ya kuwarehemu. Neno wote limetumika mara mbili katika aya hii. kuwa watu wote walivyo ni wenye dhambi, Mungu anataka awarehemu wote. Kama vile alivyowahukumu wote, ametoa rehema zake kwa wote.
Watu wote wamewekwa katika kundi moja linalofanana ili kwamba waweze kupokea wokovu unaofanana (Ona Warumi 3:19-23). Jambo la muhimu hapa ni kwamba amewaweka watu wote chini ya hukumu ili kwa njia hiyo hiyo, aweze kutoa rehema kwa watu wote.
(11:33-36) Aya hizi ni mshangao wa sifa kwa ajili ya hekima ya Mungu. Mpango mkubwa wa wokovu uko juu ya uwezo wetu kiasi ambacho hatungeweza kubuni. Tunapaswa tuupokee katika njia ile ambayo yeye mwenyewe anataka kutupa sisi, kwa sababu hatudai chochote (11:35). Watu wengine wanakwazwa na mpango wa Mungu wa wokovu, kama vile ni mwamba unaoleta kizuizi; lakini ndio jiwe kuu la msingi la rehema.
Mpango wa Mungu kwa Vipindi Maalumu (Dispensationalism) dhidi ya Teolojia ya Agano
Wanateolojia wamejaribu kuelewa uhusiano ulioko baina ya Israeli na Kanisa.
Maswali yenyewe ni pamoja na haya: Je, Watu waliokuwepo wakati wa Agano la Kale walikuwa wanaokoka kwa njia tofauti na wanavyookoka watu wa Agano Jipya? Je, ahadi za Mungu kwa Israeli zinatumika pia kwa Kanisa? Je, Israeli bado ni maalum katika mpango wa Mungu?
Mojawapo ya uhusiano kati ya Israeli na Kanisa umekuwa ukiitwa “Mpango wa Mungu.” Wanateolojia wengine wamekataa kukubaliana kwamba ni “Mpango wa Mungu” na wamekuza maelezo mengine ambayo wakati mwingine wamekuwa wakiita “Teolojia ya Agano.”
Mpango wa Mungu katika kipindi maalumu.
Mpango wa Mungu katika kipindi fulani maalumu unatokana na dhana kwamba kuna vipindi tofauti vya historia ya mwanadamu ambapo Mungu anashughulika kwa njia tofauti na watu, akitoa wokovu kupitia njia tofauti. Muda ambao Mungu anatumia mpango maalumu wa wokovu ndio unaoitwa Mpango wa Mungu katika kipindi fulani maalumu.
Baadhi ya wale wanaoamini katika mpango wa Mungu katika vipindi maalumu wanagawa historia ya mwanadamu katika vipindi maalumu. Vipindi viwili ambavyo vinaathiri sana tafsiri ya Biblia viko kwenye msingi wa tofauti kati ya Israeli na Kanisa. Waisraeli wa Agano la Kale waliokoka kufuatana na sheria ya Musa na utaratibu wa utoaji wa dhabihu mbalimbali; Waamini wa Agano Jipya wanaokolewa kwa neema kwa njia ya imani. Kanisa ni tofauti sana na Israeli, na Mungu hushughulika nao kwa pamoja kwa njia tofauti.
Ingawa kuna tofauti nyingi za dhana ya mpango wa Mungu katika vipindi maalumu, wale hasa wenye dhana hii wanafundisha kuwa ahadi zote za Mungu kwa Israeli kuhusu ardhi na ufalme zitatimizwa kiuhalisia.
Watu wanaoamini katika mpango wa Mungu katika vipindi maalumu wanafikiri kwamba mipango yote haiwezi ikafanyika kwa wakati mmoja katika dunia; kwa hiyo, wanaamini kwamba Kanisa litaondolewa duniani kwa kipindi cha miaka saba. Katika kipindi hicho, Israeli watamkubali Yesu kama Masihi wao. Baada ya kipindi hicho, kutakuwepo na kipindi kingine cha miaka 1,000 ambacho Yesu atatawala akiwa Yerusalemu.
Wanaoamini katika kipindi fulani maalumu wanalifanya Agano la Kale lisiwe na nguvu ya kutumika kwa Wakristo kwa sababu wanaamini kwamba lilikuwa limeelekezwa kwa Waisraeli tu katika kipindi kingine maalumu tofauti. Wanatumia taarifa zilizoko kwenye Agano la Kale kuelezea ukweli uliopo, lakini mara nyingi hukataa ushahidi wa mafundisho ya imani kutoka katika Agano la Kale na wanajaribu kufuata tu Agano Jipya.
Watu wengi ambao hawana ufahamu wa Mpango wa Mungu katika kipindi fulani maalumu wamekuwa wakishawishika na mawazo yake. Mara nyingi watu hukataa kukubali mamlaka ya Agano la Kale, ingawaje waandishi wa Agano Jipya kwa uhalisi walilichukulia kama ndio mamlaka yao.
Teolojia ya Agano
Kwa mujibu wa teolojia ya agano, watu wa Mungu ni wale ambao wanampenda Mungu na kumtumikia, bila kujali wanaishi katika kipindi gani cha historia. Watu waliookoka, aidha kwenye nyakati za Agano la kale au Agano Jipya, wanachukuliwa ni wale waliotubu na kumwamini Mungu kwa ajili ya wokovu.
Kwa mujibu wa teolojia ya agano, Kanisa kwa sasa ni watu wa Mungu na wanapokea ahadi zinazotolewa kwa ajli ya watu wa Mungu, ikiwa ni pamoja na ahadi zilizotolewa kwa Israeli Katika Agano la Kale. Taifa la Israeli kwa kipindi hiki halina umuhimu wowote maalumu.
Maana yeye si Myahudi aliye Myahudi kwa nje tu, wala tohara siyo ile ya nje tu katika mwili; bali yeye ni Myahudi aliye Myahudi kwa ndani, na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko; ambaye sifa yake haitoki kwa wanadamu bali kwa Mungu (Warumi 2:28-29).
Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu. Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa. Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani (Wagalatia 3:7-9).
ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani (Wagalatia 3:14).
Hapana Myahudi wala Myunani… Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi (Wagalatia 3:28-29).
Kwa mujibu wa teolojia ya agano, ahadi hizi zitatimizwa kwa kanisa badala ya Israel:
Kiti cha kifalme cha Kristo kuanzishwa Yerusalemu,
Amani
Israeli kama kiongozi wa dunia
Mataifa yote kufundishwa na Israeli
Kumilki wa milele wa nchi ya ahadi, upole wa wanyama pori.
Ahadi zote zilizotolewa kwa Israeli zimetafsiriwa kuwa na maana ya kiroho, badala ya maana halisi ya kawaida. Ahadi hizi lazima zitimizwe kwa faida ya kiroho ili zitimie kwa kanisa.
Watu wengi ambao wanaamini teolojia hii hawaamini katika utawala wa kawaida wa Kristo duniani kwa kipindi cha miaka elfu moja. Wanaamini kwamba Kristo na watakatifu wanatawala sasa kiroho kupitia ushawishi wa injili. Wanaamini kwamba ahadi kwa Ibrahimu kwamba wazao wake wataimiliki Kanani milele inakamilishwa sasa na watu walioamini na kuupokea wokovu.
Kwa mujibu wa teolojia ya Agano hakuna umuhimu wowote wa Israeli katika kipindi hiki cha sasa, kwa sababu walimkataa Kristo. Wayahudi wanaweza kuwa sehemu ya watu wa Mungu kwa kupokea wokovu binafsi, kama ilivyo kwa Wamataifa.
Uwezekano wa tafsiri nyingine
Wanateolojia wengi kwa wakati wa sasa wamejaribu kuja na mtazamo wa uwiano baina ya Mpango wa Mungu katika kipindi fulani maalumu na teolojia ya agano.
Kuna matatizo kwenye Mpango wa Mungu katika kipindi fulani maalumu. Mtume Paulo alimwambia Timotheo kwamba Maandiko ya (Agano la Kale) yalifundisha wokovu (2 Timotheo 3:15). Yesu alisema kwamba Nikodemo tayari alishajua juu ya kuzaliwa mara ya pili kwa sababu alikuwa mwalimu wa Agano la Kale (Yohane 3:10). Agano Jipya linasema kwamba mtu aliyeamini kwa sasa ni Mwisraeli wa kweli na mtoto wa Ibrahimu (Warumi 2:28-29, Wagalatia 3:28-29). Linasema pia kwamba dhabihu za Agano la Kale hazikuwa na uwezo wa kuondoa dhambi (Waebrania 10:4). Maandiko haya yanadhihirisha kuwa Mungu hajatoa njia tofauti za wokovu katika vipindi tofauti vya kihistoria.
Kuna matatizo pia kwenye teolojia ya agano. Kusema kwamba ahadi za Agano la Kale zinakamilishwa kiroho ni kuruhusu tafsiri za kufikirika ambazo haziwezi kukidhi majaribio. Pia, tafsiri hii inapoteza maana halisi ya tafsiri ya asili. Ingekuwa ni jambo lisilowezekana kwa Ibrahimu au watu wengine kuzielewa ahadi, ingawaje walifikiria kwamba walikuwa wanajua. Kwa mfano, Mungu alimwahidi Ibrahimu kwamba wazao wake watamiliki ardhi fulani milele; je hiyo inaweza ikamaanisha kwa kwamba Wamataifa wanaweza wakaokoka?
Teolojia ya agano inakataa kwamba Israeli bado muhimu kwenye mpango wa Mungu, lakini mtume Paulo alisema kwamba Waisraeli kama taifa siku moja wataokoka (Warumi 11:26).
Mtazamo wa uwiano wa Israeli na Kanisa utajumuisha ufahamu wa ahadi mbalimbali katika Agano la Kale:
1. Ahadi za Wokovu. Wokovu ni kwa neema na unapatikana kwa kutubu na imani ikiwa ni kwa Myahudi au mtu wa Wamataifa katika kipindi chochote cha historia. Msingi wa Mungu kumkubali mtu binafsi ulikuwa siku zote unafanana (Warumi 4:3, Waefeso 2:8). Hakuna haja kwa Israeli na kanisa kuwa na utengano hapa duniani kwa sababu wokovu unafanana kwa wote.
2. Ahadi za Mungu za utunzaji wa watu wake. Ahadi nyingi zinaelezea njia za kawaida za Mungu za kuwatunza watu wake, kwa yeyote ambaye yuko kwenye uhusiano wa utii na yeye. Mfano mzuri ni Zaburi ya 23. Ahadi hizi zinaonyesha asili ya Mungu Iliyofunuliwa katika uhusiano. Kanuni hizi zina matumizi yake wakati wowote na mahali popote kwa Israeli au kwa Kanisa.
3. Ahadi kwa Israeli kama Taifa. Yesu alikuwa ni Masihi kwa Wayahudi. Siku moja Israeli kama taifa litamgeukia Kristo (Warumi 11:26). Ahadi ambazo Mungu alizitoa kwa ajili ya taifa la Israeli zitaenda kutimia kama kawaida kwa ajili ya masalia ya Wayahudi walioamini.
► Je, ni taarifa gani kwenye maelezo ya uwiano yanayoendana na Mpango wa Mungu katika kipindi fulani maalumu, na ni taarifa gani zinazotofautina katika hiyo? Ni taarifa gani zinaendana na teolojia ya agano na ni zipi zinayotofautiana nayo?
Maswali ya Mapitio Somo la 10
(1) Je, jambo kuu katika Warumi 10 ni nini?
(2) Je, ni jinsi gani Wayahudi walijaribu kujihesabia haki?
(3) Je, tunajuaje kuwa watu walioishi kabla ya Kristo kuja walikuwa hawaokolewi kwa njia ya matendo?
(4) Je, ina maana gani kuwa wokovu uko mioyoni na midomoni mwetu?
(5) Je, ni kwa nini ujumbe wa mishenari ni wa haraka?
(6) Elezea mfano wa matawi ya mti katika Warumi 11.
(7) Orodhesha aina tatu za ahadi za Agano la Kale.
Kazi ya kufanya Somo la 10
(1) Andika ukurasa mmoja ukielezea ni kwa nini wakati wa leoa Agano la Kale ni muhimu kwa ajili ya Wakristo. Onyesha mifano iliyoko kwenye Maandiko ya Agano la Kale ambayo yana thamani hasa.
(2) Kumbuka kutoa taarifa ya mazungumzo yako na angalao watu wawili kutoka katika makanisa mengine.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.