Mafundisho Na Mazoezi Ya Kanisa
Mafundisho Na Mazoezi Ya Kanisa

Search Course

Type at least 3 characters to search

Search through all lessons and sections in this course

Searching...

No results found

No matches for ""

Try different keywords or check your spelling

results found

Lesson 14: Karama za Kiroho

16 min read

by Stephen Gibson


Kuorodhesha Karama za Kiroho

Tafsiri ya Karama za Kiroho

Karama ya kiroho ni uwezo aliopewa mtu aliyaemini kutoka kwa Roho Mtakatifu kwa ajili ya matumizi katika huduma ya kanisa. Ni kazi ya Roho Mtakatifu kupitia kwa mtu aliyeamini, lakini bado mtu aliyeamini hufanya uchaguzi wa jinsi ya kutumia karama yake na inawezekana pia akaitumia kwa njia isiyofaa. Karama ya kiroho siyo sawa na uwezo wa asili wa mtu, lakini karama zinaweza zikaambatana na uwezo wa asili wa mtu husika na hauwezi kutofautishwa kirahisi.

Karama za kiroho na majukumu ya huduma yameorodheshwa katika maeneo mbalimbali ya Agano Jipya. Orodha hizi ziko sawa lakini hazifanani. Biblia haijatupa sisi orodha ya karama zote za kiroho

► Mwanafunzi atapaswa kusoma Waefeso 4:7-12 kwa ajili ya kikundi.

Aya za 7-8 zinatuambia kwamba neema ya Mungu inatolewa kwa kila mtu kwa njia ya karama za kiroho. Inavyoonekana mtume hazungumzi kuhusu neema ya wokovu, kwa sababu kwenye aya ya 11 ameorodhesha majukumu ya huduma mbalimbali ambazo Mungu ametoa.

Mungu anawaita watu kwa huduma maalumu na anatoa karama za kiroho wanazozihitaji. Paulo aliorodhesha baadhi ya huduma, badala ya kuorodhesha karama za kiroho kama alivyofanya katika 1 Wakorintho. Majukumu ya huduma yaliyoorodheshwa ni mtume, nabii, mwinjilisti, mchungaji na mwalimu. Kwa hakika, haijamaanisha kuwa hii ni orodha kamili iliyokamilika ya majukumu ya huduma zote.

Mtume

Mitume walikuwa wanachaguliwa maalumu kuliendeleza kanisa baada ya huduma ya Yesu kukamilika hapa ulimwenguni. Walijulikana kwa miujiza iliyotendeka katika huduma zao (2 Wakorintho 12:12). Wote walimjua Yesu kibinafsi wakati wa huduma yake hapa ulimwenguni (1 Wakorintho 9:1, Matendo 1:21-22).

Katika kitabu cha Ufunuo tulisoma kwamba misingi kumi na miwili ya jiji iliwakilisha mitume kumi na wawili, ikimaanisha kwamba walikuwa ni watu wa kipekee kabisa katika historia ya kanisa (Ufunuo 21:14). Aya nyingine zinazoonyesha kwamba kuna mitume kumi na wawili tu ni Mathayo 10:2 na Matendo 1:26. Yuda 17 anaonyesha kwamba mitume walikuwa ni kwa siku zilizopita. Hakuna tena mitume walio hai kwa wakati wa sasa.

Nabii

Baadhi ya watu wanadhania kwamba unabii ni utabiri wa mambo yajayo, lakini Agano Jipya linarejelea kwenye kuhubiri kama unabii. Kwenye Agano la Kale, unabii mara nyingi ulijumuisha utabiri, kwa sababu hiyo ilikuwa ndiyo njia mojawapo ambayo nabii alithibitisha kwamba ujumbe wake ulikuwa unatoka kwa Mungu. Kwenye nyakati za Agano la Kale, mambo mengi yaliyoko kwenye Biblia yalikuwa bado hayajaandikwa.

Nabii ni mtu anayepokea ujumbe kutoka kwa Mungu, ambao unaweza au usiweze kujumuisha utabiri. Mamlaka ya ujumbe wake kwa kawaida ni Biblia.

Mwinjilisti

Neno mwinjilisti linatokana na neno injili. Mwinjilisti ni mtu anayewasilisha injili, aidha kwa watu binafsi au kwenye kusanyiko. Kila Mkristo anapaswa kushirikisha injili, lakini baadhi wamejaliwa kipekee kupata karama kwa ajili ya kazi hiyo. Mchungaji anapaswa kufanya uinjilisti kama sehemu ya huduma yake (2 Timotheo 4:5).

Mchungaji

Mchungaji siyo tu mhubiri, bali pia ni mtu ambaye hutoa malezi ya kiroho kwa kundi maalumu la watu.

Mwalimu

Katika kanisa, mwalimu ni mtu anayeelezea ukweli wa kibiblia na wa kiroho kwa watu wengine. Kila mchungaji anapaswa awe mwalimu (1 Timotheo 3:2, Tito 1:9), lakini watu wengine ambao siyo wachungaji wamejaliwa pia kupata karama za kuwa waalimu.

► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 12:6-8 kwa ajili ya kikundi.

Hapa mtume anasema kwamba mtu anapaswa kuelekeza juhudi zake katika karama ambayo Mungu amempa, badala ya kutawanya juhudi zake na muda wake kwenye huduma nyingi tofauti.

Baadhi ya maelekezo maalumu hutolewa kwa ajili ya aina fulani ya huduma. Kwa mfano, mtu anayeongoza ni lazima awe na bidii, na siyo kuongoza tu anapotaka kufanya hivyo, bali kuhakikisha kwamba majukumu yanatekelezwa wakati wote. Mtu anayetoa hapaswi kufanya hivyo katika njia inayomfanya aonekane bali atoe katika njia ya kawaida. Mtu anayeonesha huruma, kwa ajili ya kusaidia na hitaji la dharura anapaswa afanye hivyo kwa furaha, na siyo kwa shingo upande.

► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Wakorintho 12:28 kwa ajili ya kikundi.

Inaonekana Paulo hakukusudia kutoa orodha kamili ya karama zote au majukumu ya huduma zote katika aya hii. Kwa mfano, hakuwataja wachungaji kwenye orodha hii, ingawaje aliwataja kwenye orodha iliyoko kwenye Waefeso.

Mitume, manabii na waalimu walishajadiliwa mwanzoni katika somo hili.

Baadhi ya watu wanaitwa kwenye huduma za miujiza na uponyaji. Kila mtu aliyeamini ana fursa ya kuomba kwa ajili ya miujiza, na Mungu atajibu kwa ile imani. Hata hivyo, baadhi ya watu walioamini wanazo karama za kutambua mapenzi ya Mungu na kutumia imani kwa ajili ya miujiza.

Baadhi ya watu wanazo karama za usaidizi. Wanaona mahitaji kwa haraka zaidi kuliko watu wengine. Wanatambua nafasi za kutoa msaada kwa mahitaji ya watu binafsi au kwa kazi ya kanisa. Wanakuwa na uwezo wa aina mbalimbali wa kivitendo.

Baadhi ya watu wamepewa uwezo wa aina mbalimbali wa kuongoza na kutawala. Watu wengi wanafikiri kwamba viongozi ni watu muhimu zaidi, lakini uongozi utakuwa hauna thamani bila ya karama nyingine katika kanisa.

Karama ya lugha imeorodheshwa mwisho. Inawezekana mtume alitaka kusahihisha wale wanaofikiria kwamba hiyo ilikuwa ni karama muhimu sana kuliko nyingine.