Yonathani Edward alikuwa ni mchungaji aliyeheshimiwa na mwanateolojia aliyeishi katika miaka ya 1700. Yeye na mke wake Sara walikuwa ni wazazi wa watoto kumi na moja (11). Sara alikuwa mke na mama mzuri sana, akiwa na ushawishi mkubwa katika malezi na uundaji wa tabia za watoto wake. Mwenyewe Yonathani alikuwa ni baba aliyejitolea sana. Tunaambiwa kwamba “kila usiku wakati Bwana Edward akiwa nyumbani, atautumia muda wake wa saa moja na familia yake na kisha akiomba baraka ziwe juu ya kila mmoja.”[1]
A. E. Winship, mwelimishaji mkubwa wa mwishoni mwa miaka ya 1800 alifanya utafiti kuhusu urithi wa Yonathani na Sara Edward, akifuatilia maisha ya vizazi vyao hadi miaka 150 baada ya kifo cha Yonathani. Aligundua kwamba urithi wa Yonathani ulijumuisha yafuatayo:
Makamu wa Raisi wa Marekani - 1
Mkuu wa shule ya sheria - 1
Mkuu wa shule ya udaktari - 1
Maseneta wa Marekani - 3
Magavana - 3
Mameya -3
Maraisi wa wanafunzi Vyuo Vikuu - 13
Waamuzi - 30
Madaktari - 60
Maprofesa - 65
Maofisa wa Kijeshi - 75
Watu walioajiriwa ofisi za serikali - 80
Wanasheria - 100
Wachungaji na viongozi wengine wa makanisa -100
Wahitimu wa Vyuo Vikuu – 285
Je, urithi wenye matunda kiasi hicho unawezekanaje? Je, ni kitu gani kiliwekezwa kwenye maisha ya watoto kumi na moja wa Edward ambacho kilizalisha vizazi vilivyojulikana kwa uadilifu wao, uwajibikaji, uongozi, na huduma nyingine kwa jamii? Kwa hakika, Yonathani alikuwa baba mcha Mungu na mwenye bidii ambaye alikuwa mfano wa uaminifu kwa ajili ya watoto wake waliokuja kufuata.
Biblia Inatuonyesha kwamba uchaguzi wa wazazi huathiri uhusiano wa watoto wao na Mungu kwa vizazi vingi vinavyofuata.
► Wanafunzi wanapaswa wasome Kumbukumbu la Torati 5:9-10 na Kumbukumbu la Torati 7:9 kwa ajili ya kikundi.
Haijalishi ni uamuzi gani ambao wazazi wamefanya, kila mtu anayo nafasi ya kumtumikia Bwana na kuwa mzazi mcha Mungu kwa ajili ya watoto wake mwenyewe. Wewe na uzao wako mnaweza mkamtumikia Bwana kwa uaminifu na kupata baraka na neema zake. Je, uko tayari kujitoa kuwa mzazi ambaye unamtumikia Mungu kwa uaminifu na kuwaongoza watoto wako waweze pia kumjua yeye?
Wakati Mungu alipozungumza kwanza na Yakobo, hakusema, “Mimi ni Mungu wa ulimwengu huu,” au “Mimi ni Mungu ambaye niliumba dunia,” ingawa matamko hayo bado yangeweza kuwa ni ya kweli. Badala yake alisema, “Mimi ni Bwana, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka” (Mwanzo 28:13). Yakobo hakuanza uhusiano wake na Mungu bila ya ufahamu wa awali wa kumjua Mungu. Alijua kuhusu Mungu kwa sababu ya mafundisho ya baba na babu yake. Abrahamu alianza desturi ya kumwabudu Mungu. Watu wengine waliofuata walimwamini Mungu kwa sababu ya Abrahamu, hata kabla hawajakutana binafsi na Mungu. Wakati mtumishi wa Abrahamu Eliezeri alipoomba, alisema na Bwana, Mungu wa bwana wake Abrahamu (Mwanzo 24:12).
Baadaye Mungu alijulikana mara nyingi kama “Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo” (kwa mfano, Kutoka 3:15). Yusufu, katika kizazi kingine kilichofuata, alirejea ahadi za Mungu ambazo alikuwa amefanya na Abrahamu, Isaka na Yakobo (Mwanzo 50:24). Yusufu alitegemea familia yake iwe na uaminifu kwa Mungu sababu ya ahadi za Mungu zilizokuwa zimetolewa kwa vizazi vilivyokuwa vimetangulia.
► Kutokana na jinsi ambavyo Mungu alikuwa amejitambulisha mwenyewe, je, tunajifunza nini kuhusu njia ambazo watu walikuja kumjua Mungu?
Kwa kawaida watu hawaji kwenye uhusiano na Mungu tu kutokana na kusikia mafundisho ya imani kuhusiana na Mungu. Kwa kawaida, watu hujifunza kuhusu Mungu kwa kuangalia maisha ya watu wengine ambao wako kwenye uhusiano mzuri na Mungu. Ushawishi mkubwa zaidi hutoka kwa wazazi ambao wamejitoa kabisa kwa Mungu.
Hapa kuna baadhi ya maswali muhimu sana ya binafsi kwa ajili ya kutafakari: Je, Watoto wako wanajifunza nini kuhusu Mungu wanapotazama maisha yako? Je, watoto wako wanataka kuwa waaminifu kwa Mungu kwa sababu wanaona uhusiano wako na Mungu?
Wajibu wa Wazazi
Mungu amewapa wazazi jukumu kubwa la kufanya. “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee” (Mithali 22:6).
Wazazi wanapaswa wawe na kusudi katika kuwafundisha watoto wao kumfuata Mungu. Wazazi wanapaswa kuelewa wajibu wao wa kuongoza na kuwafundisha watoto wao.
Jukumu la kuwafundisha watoto kwanza ni la wazazi, na siyo jamii, shule au kanisa. Mzazi anapaswa ahakikishe kwamba watoto wake wako kanisani, lakini hapaswi kudhania kwamba kanisa litamfundisha mtoto wake kwa ajili yake.
► Mwanafunzi anapaswa asome Waefeso 6:1-4 kwa ajili ya kikundi.
Je, wababa wanapaswa kufanya nini?
Jukumu la kufundisha watoto siyo tu la mama peke yake. Baba pia analo jukumu la mwisho kwa ajili ya ulinzi wa kiroho wa familia yake.
Wazazi wana jukumu nyeti la kufundisha watoto wao kwa ajili ya maisha. Kufundishwa kwa ajili ya maisha haimaanishi ni kufundishwa kwa ajili ya kupata kazi; bali inamaanisha ni kufundishwa jinsi ya kuishi kwa haki, maisha ambayo Mungu atayabariki. Wazazi hawapaswi kuwaachia watoto wao kufuata dhambi, wakitumaini kwamba wanaweza wakabadilika baadaye.
Maandiko yanatuonya kwamba tusijifunze falsafa potofu za duniani.
► Mwanafunzi anapaswa asome Wakolosai 2:8 kwa ajili ya kikundi.
Andiko hili linatuonya sisi kwamba tunaweza tukaibiwa kwa kuamini falsafa potofu kukubaliana na mfumo wa maisha mabaya. Dunia inaweza kuwalaghai watoto wetu kwa kuwafundisha kufuata njia za ulimwengu badala ya kumfuata Kristo.
Ni jambo bora zaidi ikiwa elimu ambayo watoto wetu wanaipata ni kutoka kwa waalimu wa Kikristo na wazazi. Kwenye maeneo ambayo shule za Kikristo hazipo, wazazi wanapaswa kuhakikisha kwamba mtoto bado anaweza kujifunza mtazamo sahihi wa maisha.
Elimu ya dunia inaweza kumfundisha mtoto imani kwamba hakuna Mungu, mabadiliko, na ubinadamu. Watoto wako hatarini zaidi kudhurika na mafundisho potofu na au ya uongo (Waefeso 4:14), na wazazi pia ni lazima wawalinde watoto wao. Wachungaji wanapaswa wajifunze jinsi ya kufundisha mafundisho ya imani yenye uwezo wa kuwazuia watu kutenda dhidi ya falsafa za uongo. Wachungaji na waalimu wanapaswa kuwapa familia taarifa ambazo zinaweza kuwasaidia kuwaweka watoto wao kwenye ukweli.
Mafunzo ya Awali
► Mtu fulani aliandika kitabu kiitwacho Watoto ni Sementi yenye unyevu. Je, unadhani jina hili linamaanisha nini?
Wazazi wanapaswa kutambua kwamba watoto hujifunza kuhusu maisha na kuamua ni jambo lipi muhimu wangali wakiwa bado wadogo. Tabia huundwa wakati mtoto akiwa bado mdogo.
Ufuasi mwingi utatokea kabla ya watoto kufikia miaka yao ya ujana. Malengo mengi ya kifasihi ya kibiblia, malengo ya tabia, na tabia za kibinafsi, kijamii, na kiroho zinapaswa kukuzwa kabla ya miaka ya ujana.
Hata kabla ya kufikia umri wa miaka mitano (5) mtoto anakuwa ameshajifunza mambo ya misingi ya jinsi watu wanavyohusiana wenyewe mmoja kwa mwingine na ni tabia gani itakayompatia matokeo anayoyataka. Anajua kama anapaswa kutarajia haki au la, na kama adhabu na zawadi zinakuja kwa mfululizo. Anajua kama anapendwa. Anajua ikiwa hisia zake zitawafanya watu wengine wajali. Anajua kwamba anaweza kusamehewa anapokuwa amekosa. Aidha anajua kusema ukweli au kuficha makosa yake na dhambi zake. Anaweza kuamua kwamba aidha iwe au isiwe watu walioko kwenye mamlaka wanaweza kuaminika katika kumtunza na kutimiza ahadi zao.
Watoto hujifunza kutoka katika maneno na mifano ya wazazi wao, hata wakati ambapo wazazi hawajaribu kutaka kuwafundisha wao (Waefeso 5:1). Mifano ya watu wazima huwapa watoto dhana yao ya maisha. Watoto hujifunza ni jambo gani muhimu kwa kuona kile ambacho ni muhimu kwa watu wazima. Watoto hujifunza mambo ya kuwatendea watu wengine, jinsi ya kutendea kazi hali fulani zinazojitokeza, na jinsi ya kuwajibika kwa kuwatazama watu wazima. Hali hii huanzia pale mtoto anapozaliwa.
Wakati mwingine wazazi wanafikiri kwamba wanakuwa wanawafundisha pale tu wanapokuwa wamemweleza mtoto ni kitu gani afanye. Hata hivyo, mzazi anakuwa anafundisha wakati wote mtoto anapokuwa anatazama kile anachokifanya.
Mtoto hutazama watu wazima na kujifunza mambo yafuatayo: anajifunza jinsi ya kukabiliana na msongo wa mambo mengi, anajifunza jinsi ya kuwatendea watu wageni, anajifunza jinsi ya kuchukuliana na watu wa hadhi ya chini, anajifunza jinsi ya kujibu shutuma, anajifunza jinsi ya kushughulika na mahitaji ya watu wengine. Wazazi wanafundisha watoto wakati wote hata wakati ambapo hawajui kwamba wanafanya hivyo.
Endapo mtoto atakuwa anakosolewa mara kwa mara, anajifunza jinsi ya kuficha makosa yake, hutoa visingizio, na kuwalaumu wenzake. Akifikia kuwa mtu mzima atakuwa mtu wa kulaani, mnafiki na msiri sana. Ikiwa kuna migogoro ya mara kwa mara nyumbani, atakuwa na hofu na fujo. Ikiwa wanafamilia wanamdhihaki, anaweza akajiondoa kwenye kuchangamana na watu, au akawa mnyanyasaji wa watu wengine. Kama wazazi wake wanamfanya aaibike kila wakati, anajifunza kuishi na hatia, bila ya kujisikia kwamba anakubalika na Mungu. Kama atakuwa hawezi kufikia kiwango cha tabia ambacho kinahitajika na wazazi wake, hatimaye ataasi na huenda akajiunga na kikundi cha waasi wengine ambacho anakiona kama kinakuwa ni mbadala wa familia yake.
Kama watu wakiwa na subira na mtoto, anajifunza jinsi ya kuwa na subira kwa watu wengine. Kama watu watamtia moyo, anakuwa na kujiamini kwamba anaweza kujaribu. Ikiwa atapongezwa, anajisikia kuwa wa thamani sana na atakuwa tayari kutoa sifa kwa watu wengine. Ikiwa ataona haki ikitendeka, atataka naye kutenda haki.
Endapo mzazi atakuwa mtu wa kuvunja sheria na huku akimtaka mtoto wake kutii, mtoto atajifikiria kwamba siku moja na yeye atakapokuwa na umri wa mtu mzima atavunja sheria vilevile. Kama mzazi hana fadhili kwa watu wengine, mtoto anaweza kutegemea kuwa na nguvu sana za kutoweza kuwafadhili watu wengine. Kama mzazi atafikiria kwamba matatizo na mahitaji ya mtoto wake siyo muhimu, mtoto atafikiri kwamba atakapokuja kuwa mtu mzima ataweza kujihudumia yeye peke yake na kutothamini mahitaji ya watu wengine.
Kila mara wazazi wanapaswa kuonyesha utiifu wao kwa Mungu. Watoto watapaswa wajue kwamba wazazi wao wanalitii Neno la Mungu. Kama mzazi ataonyesha kwamba mapenzi yake mwenyewe ndiyo yaliyo muhimu kuliko mapenzi na au mamlaka ya Mungu, watoto wake watategemea waje kuishi hivyo. Mzazi atapaswa mara kwa aelezee kwa mtoto sababu za kufanya uamuzi na vigezo vilivyozingatiwa. Hali hii inamfundisha mtoto jinsi ya kufanya maamuzi.
Watoto hujifunza wakati wazazi wao wanapokuwa wanacheza nao. Wanatakiwa wajifunze kuhusu haki, wema, na kuwa na majibu kwa watu wengine. Michezo hukuza ujuzi wa mtoto. Madhumuni ya michezo ya familia ni pamoja na kujifunza, maendeleo binafsi, na kufurahia mahusiano na wanafamilia wengine. Mashindano kwenye michezo ya familia ni mazuri lakini hayapaswi yawe ni kwa sababu kuwatawala wengine ili mshindi aweze kufurahia kuwa bora zaidi kuliko mwingine. Swali la kutafakari wakati wa mchezo ni hili, “Je, kila mtu anafurahia mchezo?” Iwapo mshindi pekee ndiye atakayekuwa anafurahia mchezo, makusudi yasiyo sahihi yanatekelezwa. Kama watu wanapatwa na hasira wakati wa mchezo, mchezo huo haupo kwa ajili ya kukidhi makusudi yaliyo sahihi.
Wazazi hudhihirisha thamani ya mtoto wao wanapotumia muda wao pamoja na shughuli za mtoto. Wazazi wanapaswa wamsaidie mtoto wao katika miradi ya shule, kutengeneza au kufanyia ukarabati vifaa vyake vya kuchezea, na kumpa nafasi ya kibinafsi nyumbani, kusikiliza hadithi zake na vichekesho vyake, na kumfariji anapokuwa amefadhaika.
Wazazi wanapaswa wawajue waalimu wa mtoto wao. Wanapaswa wahudhurie kwenye kila mkutano ulioratibiwa kwa ajili ya kukutana na waalimu ili kujua hali ya mtoto inavyoendelea shuleni. Kama kuna uwezekano, wazazi wote wawili wanapaswa wahudhurie kwenye mkutano huo. Kama baba hataweza kushiriki katika kikao hicho, inakuwa na maana kwamba mambo mengine anayoshughulikia ni ya maana zaidi kuliko mtoto wake. Wazazi wanapaswa wawaulize na au wawahoji waalimu kuhusu ufaulu wa mtoto na mambo mengine yanayoendelea hapo shuleni. Waalimu wanategemewa wafanye mambo mazuri kwa mtoto kadri ya uwezo wao na kumlinda mtoto dhidi ya kutendewa mambo mabaya ya unyanyasaji ikiwa wanajua kwamba wazazi wa mtoto wanapendezwa na hatua hiyo.
Watu wanaoishi pamoja kama familia wanajuana vizuri sana. Wanajifunza mahitaji na makosa ya kila upande. Wanaweza wakapendana na kudhihirisha kwamba upendo huo ni zaidi ya wanavyoweza kumpenda mtu mwingine yeyote katika dunia. Kama hawawezi kupendana, wanaweza wakaumizana kwa njia nyingi kuliko mtu mwingine yeyote. Watu wengine huwatendea familia zao vibaya kabisa kulikoni hata wanavyowatendea watu wengine wasiowajua. Kwenye nyumba ya Kikristo inapaswa pawe ni mahali pa kuonyesha ustahimilivu, msamaha, utunzaji, na wema.
Ajira kwa Watoto
Mtoto mdogo anahitaji muda wa kucheza na burudani kila siku. Mtoto anahitaji muda wa kupumzika, kutumia mawazo yake, kusoma vitabu, kucheza, kutengeneza vitu vyake au kujenga kitu, na kufurahia mazingira ya asili. Katika hali ambayo familia hufanya kazi pamoja kila siku katika kuzalisha chakula au kufanya majukumu mengine, inaweza kuwa ni jambo zuri kwa watoto kushirikishwa katika kazi za familia, lakini wazazi wanapaswa kukumbuka maadili mengine pia.
[1]masaa mengi kazini ni ngumu kwa mtoto sio tu kwa sababu ya mahitaji ya mwili, lakini kwa sababu kazi anayopewa mtoto kwa kawaida ni ya kurudia-rudiwa na ya kuchosha. Anatamani kupata muda kwa shughuli zinazotumia mawazo yake. Inasikitisha ikiwa mtoto lazima afanye kazi nyingi sana kiasi kwamba wakati wake pekee wa burudani ni anautumia kwa ajili ya kula na kulala ili aweze kufanya kazi tena.
Baadhi ya familia zinapitia katika hali ngumu kiuchumi na kuwa na fikra kwamba zinahitaji msaada wa kipato kutokana na kazi za watoto wao. Hata hivyo, ikiwa wanashindwa kuwasomesha watoto wao, huenda hali ya familia yao isibadilike kamwe. Kama mtoto atakuwa anafanya kazi badala ya kwenda shule, labda atatumia maisha yake yote kwenye kazi zenye ujira mdogo tu au kazi za vibarua. Kazi nyingi na fursa za kibiashara hazitaweza kupatikana kwa ajili yake.
Baadhi ya watu hutoa elimu kwa watoto wao wenyewe lakini wako tayari kuwatumia vibaya watoto wa familia maskini kwa kuwaajiri kwa masaa mengi kwenye mashamba au kazi za nyumbani, au katika biashara ya kuuza mtaani, huku wakijua kwamba hawakuwahi kupatiwa elimu. Wakristo wanapaswa kushirikiana kwa pamoja ili kutafuta suluhisho lililo bora kwa ajili ya familia zilizoko katika jamii zao.
Watoto wanaweza kufurahia kazi ikiwa wanapewa majukumu yanayowapa hisia ya mafanikio. Pia Wanaweza kufurahia kufanya kazi na wazazi wao ikiwa wazazi watawatia moyo. Wazazi wanapaswa matarajio ya kimaendeleo juu ya kile ambacho mtoto anaweza kufanya na watoe mrejesho wa kujenga kwa njia chanya ili mtoto ahamasike kuendelea kujifunza na kukua.
Ni jambo zuri kwa watoto kuwa na majukumu ya kufanya kila siku ya kuwafundisha kuwa watu wa kutegemewa na wa wazi. Wazazi wanapaswa wawathibitishie kwa maneno ya kutamkwa wazi kuhusu sifa za tabia wanazoziona kwa mtoto anapokuwa anafanya kazi, kama vile, uwezo wa kuanzishia mambo au kuvumbua njia, kufanya kwa bidii, uangalifu, na ustahimilivu. Wazazi wanapaswa wawafundishe watoto wao kanuni za kazi zinazofundishwa katika Neno la Mungu.
Ni jambo zuri kwa watoto kuwa na fursa za kujipatia fedha ambazo wanaweza wakajichagulia namna ya kuzitumia. Wanajifunza thamani ya kazi yao na wanajifunza jinsi ya kutumia fedha zao kwa njia ya faida nzuri na bora zaidi. Mtoto anayefanya kazi ili kupata fedha anaweza akajitambua kwamba hapaswi kuzitumia zote kwa ajili ya kununulia pipi; atataka anunue kitu ambacho anaweza akakihifadhi mwenyewe. Wazazi wanapaswa kuwafundisha watoto wao kufikiri kuhusu fedha na namna ya kuzitumia kwa njia za kimungu.
Ni jambo zuri kwa watoto na vijana kutambulishwa kwenye aina mbalimbali za kazi ambazo zinaweza kuendeleza uwezo wao. Ni jambo zuri ikiwa kijana mdogo atakuwa na fursa ya kufanya kazi na watu wa aina mbalimbali wenye vipaji vinavyotofautiana ili aweze kujifunza.
► Je, ajira za watoto zilizopo katika jamii yenu ni za hali gani? Je, wazazi wawe wakifanya nini? Je, kanisa liwe likifanya nini?
“Wakati mtu anapokuwa hana tena huruma kwa vijana, manufaa yake duniani yanakaribia kumalizika.”
- George MacDonald
Makusudio ya Maendeleo ya Mtoto
Wazazi wanalo jukumu la kukuza tabia ya mtoto wao. Wanandoa fulani wa Kikristo, Matt na Mariamu Friedeman, waliorodhesha sifa ambazo walitaka ziwasaidie watoto wao kustawi. Baada ya kutengeneza orodha hiyo, waliikagua na kutengeneza mipango kwa ajili ya hatua ambazo zingesaidia watoto wao kukua kupitia kwenye kila kipengele cha sifa hizi. Mchakato wenyewe haupaswi uwe wa haraka. Sifa hizi hazijitokezi kwa ghafla. Wazazi wanapaswa kuwa na makusudio na mwelekeo thabiti katika miaka yote ya kuwalea watoto wao. Orodha iliyoko hapa chini ni baadhi ya sifa zilizoorodheshwa na Friedemans.[1] Sifa nyingine zimeongezwa kwenye orodha hiyo.
Aina
Sifa za kuwa nazo ifikapo umri wa miaka 18
Kiroho
Kufahamu kwamba wao ni wabebaji wa sura ya Mungu pamoja na thamani ya umilele.
Kufahamu kwamba wao ni wenye dhambi wanaomhitaji Mwokozi.
Kuamua kujitoa kabisa kwa Kristo
Kuwa na maisha ya ibada kila siku
Kufanyia kazi karama za Kiroho
Kuwa tayari kwa ajili ya huduma ya Kikristo
Kubakia wasafi bila kujamiiana hadi wafikie ndoa
Elimu ya Biblia
Kuelewa mafundisho ya msingi ya imani za Kikristo
Kuweza kukariri maandiko muhimu (Aya 300)
Kujua hadithi za Biblia
Kujua vitabu vyote vilivyoko katika Biblia
Kujua Amri zote Kumi za Mungu na Hotuba ya Mlimani ya Yesu
Kutambua mada za Injili zinazohusiana na dhambi na wokovu katika Biblia nzima
Mtazamo wa dunia wa Biblia
Kufahamu jinsi ya kutetea imani yao
Kuwa na uwezo wa kujibu hoja kubwa za maisha kutoka katika mtazamo wa Kibiblia
Kufahamu ni nini kinachofanya Ukristo uwe wa kipekee miongoni mwa dini zote na madhehebu yote ya dunia
Uwezo wa Kufikiri (Elimu)
Kupata elimu ya Kikristo kama uwezekano utakuwepo
Kuanzishiwa nidhamu ya kusoma au kusikiliza podikasti au video za kufundishia
Kuhudhuria chuo cha Biblia au vituo vya mafunzo ya taaluma, kulingana na vipaji vyao na wito wao
Tabia
Kufanya mazoezi ya Kujidhibiti mwenyewe
Kuwa mnyenyekevu-na uwezo wa kuomba msamaha
Kuonyesha heshima kwa mamlaka zilizopo
Kuongea kwa wema
Kujifunza jinsi ya kuenenda na kutumia muda kwa busara—wao wenyewe kujiweka katika nidhamu ya matumizi ya vyombo vya habari vya kijamii, burudani na mengineyo
Fedha na Huduma
Kufahamu kuhusika kwa Mungu kwa ajili ya watu maskini
Kuwa wakarimu na kuwahudumia maskini
Kuwa watoaji wa mafungu ya kumi na kuweka akiba
Wajifunze jinsi ya kutumia bajeti ya fedha
Mahusiano
Kuonyesha upendo na kuambatana na ndugu
Kudhihirisha adabu ya kawaida katika mpangilio mzima wa kijamii
Kujifunza jinsi ya kuwa rafiki mwaminifu
Kuwa na uwezo wa kuzungumza na watu wazima kwa heshima na kujiamini
Afya
Kufanyia mazoezi tabia nzuri ya usafi
Kufanya mazoezi ya mwili ya mara kwa mara
Kula chakula chochote kinachopatikana kwa ajili yao
Kuchagua chakula kilicho bora kila inapowezekana
Ujuzi
Kuendeleza ujuzi na vipaji ambavyo Mungu amewapa
Kuendeleza ujuzi na vipaji vyao kupitia nidhamu ya mazoezi endelevu ya mara kwa mara
Matt Friedeman alielezea kile walichokifanya yeye na mke wake baada ya kuwa wameorodhesha sifa hizi:
Mara tu baada ya kuwa na sifa hizo hapo juu kwenye karatasi yetu, tulichora mstari katikati ya karatasi na tukajiuliza wenyewe, “Sasa tunatakiwa tufanye nini [tufanye sehemu yetu ya kuendeleza sifa hizi kwa watoto wetu]?” Kwenye upande wa kushoto wa karatasi, tuliandika hapo majukumu [yetu] ya wazazi.[2]
Ikiwa hili litaonekana kama ni jukumu kubwa, kumbuka tu kwamba Mungu ametupa sisi miaka ya 16-18 ya kufanya uanafunzi kwa ajili ya watoto wetu.
Ni muhimu:
1. Kutekeleza mapango wa mwanafunzi.
2. Kuanzisha ratiba za mazoea za kifamilia, kama vile kupata chakula au mlo wa kila siku na dakika chache za mafundisho/mafunzo yaliyopangwa.
3. Kufanya uanafunzi kama sehemu ya maisha ya kila siku, kwa kutumia fursa nyingi za mafundisho na mafunzo.
4. Kuendelea kuombea watoto wako kwa kutumia Neno la Mungu.
5. Usikate tamaa hata pale unapoona umeshindwa.
► Chagua vipengele vichache kutoka kwenye jedwali lililopo hapo juu na uelezee ni nini ambacho wazazi wanaweza kufanya kwa makusudio ya kufikia malengo hayo.
[1]Matt Friedeman, Discipleship in the Home, (Wilmore: Francis Asbury Society, 2010), 31-33.
[2]Matt Friedeman, Discipleship in the Home, (Wilmore: Francis Asbury Society, 2010), 33.
Kipengele cha Mapenzi ya Mwanadamu.
► Wakati mwingine mtu husema, “Matukio niliyokutana nayo yamenifanya kuwa aina ya mtu nilivyo sasa.” Kauli nyingine inayofanana na hiyo ni, “Mtu alivyo ni matokeo ya mazingira yake mwenyewe.” Je, hizi kauli zina ukweli?
Wanadamu wameumbwa kwa sura ya Mungu. Watu hufanya maamuzi ya uhakika na siyo ya kudhibitiwa na silika au mazingira. Katika maandiko yote Mungu amewaita watu kuchagua aidha kufanya mambo yaliyo mema na kukataa maovu.[1] Mungu huwahukumu watu kutokana na maamuzi yao.
Mazingira na uzoefu wetu wa mambo mbalimbali hutushawishi sisi, lakini havina uwezo wa kutudhibiti kwa sababu kama wanadamu tulio katika sura ya Mungu tunafanya maamuzi ya uhakika. Hiyo inamaanisha kwamba hatimaye mtoto anaweza kufanya maamuzi yake mwenyewe yanayotofautiana na ya nyumba na mazingira aliyolelewa. Mtoto aliyetoka katika nyumba ya upagani ambako maisha ya dhambi yalikuwa ni jambo la kawaida kwao anaweza akatubu na akaishi kwa ajili ya Mungu. Mtoto aliyetoka katika nyumba ya Kikristo anaweza akachagua kuishi kwa kutokumfuata Mungu.
Ingawa watu hufanya maamuzi ya uhakika, siyo kwamba wako huru kabisa. Biblia inatuambia kwamba tunazaliwa na asili ambayo ina mwelekeo wa kutenda dhambi (Zaburi 51:5, Zaburi 58:3). Wanadamu wana mwelekeo wa asili wa kupingana na mamlaka, kuchagua mwelekeo wao wenyewe, kujiingiza kwenye majaribu, kudanganya watu wengine, na kuwa wabinafsi (Waefeso 2:1-3).
Watoto hutafuta kwa haraka njia za kutekeleza matamanio yao binafsi hata kama itakuwa ni lazima wadanganye na kutotii ili kupata kile wanachokihitaji. Zaidi ya hapo, tunajua kwamba Shetani hujaribu kuwadanganya na kuwajaribu (Waefeso 2:2, Ufunuo 12:9).
Wazazi ni lazima watambue kwamba maelekezo pekee hayatoshi kumfanya mtoto afanye atende haki. Kuna mapambano ya kiroho (Wagalatia 5:17). Wazazi wanapaswa waombe ili Roho wa Mungu aweze kumshawishi na kumwongoza mtoto. Wazazi wanapaswa kumtegemea Mungu kwa ajili ya hekima na kwa ajili ya kupata nguvu ya kuwa mifano mizuri ya kiroho. Wazazi wanapaswa kuomba bila kukoma na au kwa bidii ili kwamba watoto wao waweze kutubu na kuweza kuzaliwa upya kiroho katika umri mdogo.
Hata kama mtoto ameokoka, mzazi hapaswi kutarajia kuwa mtoto wake atakuwa anafanana na Mkristo aliyekomaa. Tabia zake na hisia zake hazitakuwa sawa. Wakati mwingine anaweza akajiingiza kwenye majaribu. maadamu mtoto anaonyesha nia ya kutenda mambo mema, mzazi hapaswi kumkatisha tamaa kwa kumwambia kwamba anashindwa kuishi kama Mkristo. Badala yake, mzazi anapaswa kumpongeza mtoto kwa mambo yake mema anayofanya kama Mkristo na kumtia moyo wa kuomba kwa ajili ya kumsaidia katika mapambano yake.
Ingawa kila mwanadamu amezaliwa akiwa na mwelekeo wa kutenda dhambi, kila mwanadamu pia anamhitaji Mungu. Roho Mtakatifu huzungumza na kila mtu na kutoa matamanio ya kuwa kwenye uhusiano na Mungu. Tunajua kwamba tunasaidiwa na Mungu tunapokuwa tunawafundisha watoto wetu Neno la Mungu. Roho wa Mungu ni kama wakili aliye ndani ya mtoto, akithibitisha kuhusu ukweli na kumpa matamanio ya kuwa kwenye uhusiano na Mungu.
Familia zinapaswa kukutana kila siku kwa dakika chache kwa ajili ya usomaji wa Biblia, majadiliano, na maombi. Wazazi wote pamoja na watoto wote walioko kwenye nyumba wanatakiwa wahudhurie. Baba anapaswa kuongoza, lakini anaweza kuwataka wanafamilia kusoma maandiko na kushiriki kwa njia nyingine mbalimbali.
Muda wa ibada siyo lazima ufuate mtindo au utaratibu wa kila siku unaofanana. Muda huu unaweza kuwa na miundo mbalimbali ya ibada, na unaweza ukajumuisha kusoma hadithi za Biblia, hadithi za historia ya Kikristo na umisheni, kujadili maswali yaliyoulizwa, matumizi ya maswali ya kukariri, na majibu ya kufundisha kweli za mafundisho ya imani, kusoma Maandiko mbalimbali yanayohusiana na Ukristo nyimbo, kukariri Biblia, maigizo, na njia mbalimbali za kufanya maombi.
Mfano wa wakati wa shughuli ya ibada: Chagua hadithi ya Biblia na waambie wanafamilia waigize.
Wachungaji wanapaswa watumie sehemu ya muda wao kufundisha kanisa kuhusu muda wa ibada wa familia. Wazazi wanapaswa wakumbuke kwamba Mungu amewapa jukumu la kuwafundisha watoto wao Neno la Mungu (Kumbukumbu la Torati 6:5-7).
Kwa ajili ya Majadiliano ya Kikundi
► Je, kuna dhana gani kutoka katika somo hili ambazo ni mpya kwako? Je, umejipangaje kuutumia ukweli ulioujifunza?
► Je, kanisa linaweza kufanya nini ili kuimarisha familia na kuwasaidia wazazi katika kulea mtoto?
► Je, watu wa kanisa wanawezaje kufanya kazi kwa pamoja li kusaidia katika changamoto ya kufundisha watoto ili wamfuate Kristo?
► Je, kuna baadhi gani ya mifano ya mazoea ya kila siku ambayo familia zinapaswa kufuata?
Maombi
Baba wa Mbinguni,
Asante kwa kuunda familia na kuwapa watu upendeleo mkubwa wa kuwa wazazi.
Tusaidie kuwapenda watoto wetu kama wewe unavyofanya. Tusaidie kukumbuka daima kwamba wameumbwa kukujua na kukutumikia wewe.
Tupe upendo, subira na ufahamu tunaohitajiili kwamba tuwafundishe na kuwashawishi watoto wakufuate wewe.
Wawezeshe waumini ndani ya makanisa yetu kuweza kuwatayarisha familia, vijana, na watoto kuwa na nguvu katika imani na utii.
Ameni
Kazi za Kufanya
(1) Soma kila moja ya kipengele cha Aya zinazofuata. Tumia aya hizi kuandika kurasa tatu kuhusu kile ambacho andiko linafundisha kuhusu wajibu wa wazazi:
Mwanzo 18:17-19
Kumbukumbu la Torati 6:4-9
Zaburi 78:1-8
Wakolosai 3:21
Waefeso 6:4
1 Timotheo 3:4-5, 12
2 Timotheo 3:14-17
Mathayo 18:5-6
(2) Aidha wewe ni mzazi au siyo, chagua sifa tano kutoka katika mojawapo ya malengo yaliyoorodheshwa katika jedwali lililotolewa katika somo hili. Andika njia tatu za vitendo zinazofaa za kuwasaidia watoto wako kufikia kila moja ya malengo matano ya sifa zilizochaguliwa.
(3) Kama wewe ni mzazi, andika mpango na ahadi yako ya kuwa na ibada za kila siku pamoja na watoto wako. Jiwajibishe mwenyewe kwa mtu mwingine kwa ajili ya mpango na ahadi ambayo umeifanya.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.