Malengo ya Somo
Hadi kufikia mwishoni mwa somo hili, mwanafunzi atapaswa:
(1) Kuelewa na kujibu utasa kutoka kwa mtazamo wa kibiblia.
(2) Kumthamini kila mtu kama aliyechuka sura ya Mungu.
Search through all lessons and sections in this course
Searching...
No results found
No matches for ""
Try different keywords or check your spelling
20 min read
by Stephen Gibson
Hadi kufikia mwishoni mwa somo hili, mwanafunzi atapaswa:
(1) Kuelewa na kujibu utasa kutoka kwa mtazamo wa kibiblia.
(2) Kumthamini kila mtu kama aliyechuka sura ya Mungu.
Busaba alikuwa ni msichana aliyezaliwa katika nchi moja ya Asia. Alifurahi alipoolewa na mfanyabiashara kijana, na walitegemea kuwa na maisha ya furaha wakiwa pamoja. Miaka kadhaa ilipita, na Busaba alikuwa bado hajabahatika kupata watoto. Daktari aliwaambia kwamba Busaba hangekuwa na uwezo wa kupata watoto. Mume wake alijawa na masikitiko mengi na hasira kali. Mwisho wa mambo yote aliamua kumpa Busaba talaka na akamwoa mwanamke mwingine. Busaba sasa ni mzee. Anaishi kwenye nyumba ndogo yeye mwenyewe na hana jamii inayoshughulika naye katika maisha yake. Kwa kuwa yeye ni wa dini ya Bhudha, ana mategemeo kwamba siku moja katika maisha ya baadaye atakuwa na watoto na aibu yake itakuwa imekoma na au imefikia mwisho.
► Je, kama wewe ungelikuwa ni mchungaji kwenye jamii ya Busaba, ungelisema nini na yeye? Je, ujumbe wa Kristo kwa Busaba ni nini?
Kwenye somo hili au mafundisho haya tunaenda kuangalia mtazamo wa kibiblia kuhusiana na suala la kukosa mtoto.
Mara tu baada ya Mungu kumuumba mwanamume na mwanamke wa kwanza, aliwaambia kwamba wazae watoto, waongezeke, na wakaijaze nchi (Mwanzo 1:28).
Kwenye Agano la Kale, wakati mwingine Mungu alitoa ahadi za baraka siyo tu kwa mtu binafsi bali kwa vizazi vingi vya familia. Kwa mfano, Mungu aliahidi baraka kwa Ibrahimu ambazo hazikuja tu kwa Abrahamu mwenyewe bali pia kwa vizazi vyake vya baadaye. Mungu alikuwa amemuahidi Abrahamu kwamba wazao wake wangekuwa wengi kama mchanga wa bahari. Mimba ya mtoto wa Ibrahimu aitwaye Isaka ilipatikana kimiujiza. Kisha kwa kadri familia ilivyokuwa inaongezeka kwenye kila kizazi, idadi ikaongezeka ikiwa ni udhihirisho kwamba Mungu alikuwa anatimiza ahadi yake.
Katika Kutoka 23:25-27 Mungu aliwaambia Waisraeli kwamba atawabariki watakapokuwa wanaingia katika nchi yao mpya. Mungu aliwaahidi Waisraeli kwamba atabariki vyakula vyao, atawaondolea magonjwa, hataruhusu utasa au kuharibika kwa mimba, na kuwaharibu maadui zao. Ahadi hizi zilitegemea utiifu wa Waisraeli, na Mungu akafafanua mahitaji yake kwao (kama vile amri iliyoko katika Kutoka 23:32). Ahadi hizo zilikuwa zimetolewa kwa ajili ya taifa zima la Israeli na siyo kwa ajili ya watu binafsi. Watu binafsi wangehusishwa na kutii au kutotii kwa taifa. Kwa mfano, mtu anaweza kuwa mgonjwa, au mwanamke akawa hana watoto, siyo kwa sababu ya dhambi zao wenyewe, bali ni kwa sababu walikuwa kwenye taifa ambalo halikuwa mwaminifu kwa Mungu. Kwa hiyo, mwanamke ambaye hakuwa na mtoto huenda asiwe anateseka kutokana na matokeo ya dhambi zake mwenyewe.
Kumbukumbu la Torati 7:12-15 ni kifungu chenye ahadi kwa taifa la Israeli. Kutakuwepo na mafanikio, hakuna magonjwa, na hakuna utasa kwa wanadamu au wanyama. Aya ya 12 inasema kwamba Waisraeli watapokea baraka hizi kama watamtii Mungu kwa sababu Mungu alifanya maagano na babu zao. Mtu aliyeko Israeli anaweza kuwa maskini, au mwanamke anaweza kukosa mtoto, kama taifa halikuwa na uaminifu kwa Mungu.
Watoto walikuwa muhimu katika mpango wa Mungu kwa ajili ya watu wake. Katika sehemu nyingine za kozi hii, tulizungumza kuhusu jinsi ambavyo watoto wanapaswa kuthaminiwa kwa sababu wameumbwa katika sura ya Mungu. Kila mtoto ni wa thamani na anapaswa kutendewa kwa upendo na kutunzwa. Hata hivyo, wakati mwingine watu huhisia kwamba mtoto ni wa thamani kwa sababu anaweza kuifanya familia ikawa imara katika siku za baadaye. Wakati mwingine baba huwathamini watoto kwa sababu ni sehemu ya mwendelezo wa utambulisho wake yeye mwenyewe. Tunapaswa tukumbuke kwamba Mungu hutupatia watoto kwa ajili ya malengo yake mwenyewe (Malaki 2:15).
► Kikundi kitapaswa kiangalie katika Zaburi 127:3-5 kwa pamoja na mtu akiwa anasoma kwa sauti.
Kifungu hiki katika Biblia kinasema kwamba watoto ni baraka kutoka kwa Mungu. Ni kama urithi ambao Mungu ameubariki. Ni zawadi kutoka kwa Mungu. Ni walinzi na usalama wa familia zijazo.
Baraka za aina mbili ambazo wakati mwingine huzungumziwa kwa pamoja katika Maandiko ni maisha marefu na uzao wa wajukuu. Ayubu alibarikiwa kwa sababu alikuwa na watoto kumi na aliishi maisha marefu ya kutosha kiasi ambacho aliona vizazi vyake vinne (Ayubu 42:13, 16). Baraka zilizoko katika Zaburi 128:6 ni zawadi ya kuishi ili kuweza kuona wajukuu zako.
Mungu alibariki familia ya Yonadabu kwa ahadi kwamba daima kutakuwepo na mtu wa kuongoza kizazi kitakachofuata cha familia (Yeremia 35:19). Mungu alitoa ahadi kwa familia ya Mfalme Daudi kwamba siku zote atakuwa na mtu atakayekaa kwenye kiti cha enzi cha ufalme (2 Samuel 7:16).
Kwa hiyo tunaona kwamba baraka za Mungu kwa ajili ya familia kwa kawaida huhusisha watoto, na ni njia ambayo baraka za Mungu zinaendelezwa hadi kwenye vizazi vya baadaye.
Ugumba/kukosa mtoto katika visa vingine inamaanisha kwamba Mungu ameilaani familia. Biblia inatueleza kuhusu matukio ambayo Mungu alizilaani familia kwa ugumba. Kwa mfano, kwa kuwa mfalme Abimeleki alitenda makosa, Mungu alizuia wanawake wote wa nyumba yake wasipate watoto hadi aliporekebisha makosa yake (Mwanzo 20:18). Wanawake katika jambo hili hawakuwa na hatia, lakini walipata matokeo ya dhambi ya mfalme.
Baada ya Adamu na Hawa kutenda dhambi, Mungu alisema kwamba dunia ingeathiriwa kutokana na dhambi yao. Laana iliyotolewa ilihusisha pamoja na mambo mengine, mahusiano magumu ya kibinadamu, kuzidishiwa uchungu na utungu wa kuzaa watoto, kazi ngumu, upinzani wa ardhi katika kilimo, na mwishowe kifo (Mwanzo 3:14-19). Kila mwanadamu kuanzia wakati wa Adamu amekuwa katika hali ya dhambi kuanzia siku anapozaliwa, hata kabla hajatenda dhambi kwa binafsi yake yeye mwenyewe. Hata Yesu, ambaye hakuwahi kuwa na dhambi kabisa, aliingia katika uumbaji wa dunia akiwa katika mwili wa mwanadamu uliokuwa katika hali ya laana. Kwa hiyo, hatupaswi kusema kwamba mateso ya mtu binafsi ni matokeo ya dhambi yake mwenyewe. Watu wote tunazeeka, tunapatwa na magonjwa, tunakutana na mateso kwa njia mbalimbali, na hatimaye tunakufa. Matatizo haya yote, ikiwa ni pamoja na matatizo ya kutokupata watoto/ugumba, ni matokeo ya dhambi ya kwanza ya Adamu.
Mbali na dhambi ya asili ya Adamu, tunaathiriwa na dhambi za wazee wetu, kwa sababu matendo yao yalitengeneza jamii ambayo ndiko tulimozaliwa. Tumeathiriwa na dhambi za familia zetu, jamii, na taifa. Waumini kila mahali duniani wamekumbana na hali ambazo zimetengenezwa na jamii wasiyoidhibiti. Familia inaweza ikajikuta katika hali ya umaskini kwa sababu wako kwenye sehemu ambayo ina uhuru kidogo na fursa. Mtoto mchanga anaweza akazaliwa akiwa na ulemavu wa mwili ingawaje hajawahi kufanya uchaguzi wowote wa kutenda dhambi (Yohana 9:1-3).
Mungu hafanyi maamuzi kuhusu kutupa watoto kwa ajili ya sababu ambazo tunaweza kuwa na ufahamu nazo. Wakati mwingine watu wanaoishi maisha ya uzembe, ya uasi wa dhambi wanakuwa na watoto wengi na hawana mpango wa kuwalea katika njia ambazo zinampa Mungu utukufu (Zaburi 17:14). Wakati mwingine waumini walio waaminifu kabisa hawajawahi kupata watoto. Kwa hakika, hatupaswi kudhania kwamba dhambi fulani ya mtu ndiyo iliyosababisha ugumba au kutopata mtoto.
Tunajua kwamba Mungu anao uwezo wa kuingilia kati kwa uponyaji na baraka zake wakati wowote anaochagua, lakini kwa ujumla, waumini huvumilia hali zote za ulimwengu. Tunasubiri kwa imani wakati ambapo Mungu atafanya upya tena uumbaji wake (Warumi 8:18-23).
Siyo haki kumlaumu mwanamke kwa kutokuwa na mtoto, kana kwamba dhambi yake mwenyewe ndiyo iliyomsababishia laana. Vivyo hivyo, mtoto mtarajiwa anapokufa kabla hajazaliwa, kifo hicho kwa kawaida siyo kwa sababu ya jambo lolote ambalo mama yake atakuwa amelitenda. Watu binafsi wanapitia mateso kwa njia mbalimbali kutokana na dhambi ya Adamu, dhambi za watu wengine, na hali ya ujumla ya dunia ilivyo. Kwa kuwa kila mmoja ametenda dhambi, ubinadamu unashirikishana kwa pamoja hatia kwa ajili ya hali ya ulimwengu, lakini watu binafsi wanapitia mateso kwa njia mbalimbali mahususi.
Yesu alidhihirisha upendo wa Mungu wakati alipoponya na kutenda miujiza mingine mingi. Katika historia yote iliyoandikwa katika Biblia, tunaona miujiza mingi ya Mungu iliyofanyika kwa ajili ya watu wake.
Mungu anataka sisi tuishi kwa furaha na bila mateso katika dunia hii ya uzuri (Mwanzo 1:28, 31, 1 Timotheo 6:17). Hata hivyo, kipaumbele cha kwanza kabisa cha Mungu ni kutuokoa katika dhambi ili tuweze kufurahia uhusiano wa milele pamoja naye. Wokovu kwa ajili ya wenye dhambi huchukua muda kwa sababu watu ni lazima wachukue maamuzi ya kutubu na kuamini. Kama Mungu angeamua kumaliza maumivu na mateso yote kwa sasa, ni watu wachache sana watakaotubu, kwa sababu watakuwa hawajui ubaya wa dhambi. Kwa hiyo, kwa sasa hivi, mateso ni lazima yaendelee wakati Injili ikiwa inahubiriwa kila mahali duniani. Hatuwezi tukategemea miujiza iwe ndiyo utatuzi wa matatizo yetu yote na iondoe maumivu yetu yote, ingawaje mara chache hufanya miujiza kwa ajili yetu.
Mwishowe, mateso yote yataisha kwa wale wote ambao watakuja kwenye uhusiano binafsi na Mungu. Lakini kwa wakati huu, Mungu anahuzunika pamoja nasi katika mateso yetu (Yohana 11:35), na hutufariji kwa njia nyingi (2 Wakorintho 1:3-7).
Mojawapo ya miujiza ya Mungu ni kumfanya mwanamke asiyekuwa na mtoto aweze kuwa mama mwenye watoto (Zaburi 113:9).
Biblia ina kumbukumbu zilizoandikwa sizizopungua sita ambazo Mungu amempa mtoto mwanamke ambaye hakuwahi kuwa na mtoto hapo kabla. Ingawaje Mungu amefanya miujiza hii mara nyingi, hizi za mara sita zilinukuliwa kwa sababu watoto walikuwa ni muhimu kwa ajili ya historia: Isaka alizaliwa na Sara (Mwanzo 21:1-3). Yakobo na Esau walizaliwa na Rebeka (Mwanzo 25:21, 25-26). Yusufu alizaliwa na Raheli (Mwanzo 30:22-24). Samsoni alizaliwa na mke wa Manoa (Waamuzi 13:2-3, 24). Samweli alizaliwa na Hanna (1 Samweli 1:20). Yohana alizaliwa na Elizabethi (Luka 1:13, 57).
Katika kila moja ya matukio haya sita, wanandoa walikuwa wamepitia katika kipindi cha huzuni kwa sababu mke alikuwa hajajaliwa kupata mtoto. Kwenye kumbukumbu za Biblia, Mungu hakuwahi kumlaumu hata mmoja wao kwa ajili ya mwanamke kukosa mtoto. Biblia haionyeshi mahali popote kwamba Mungu hakuwa amependezwa na mmojawapo wa mzazi yeyote kati ya hawa sita. Luka 1:5-7 anasema kwamba Zakaria na Elizabethi walikuwa watu wenye haki mbele za Mungu, wakitii kwa ukamilifu wote amri na maagizo yake, lakini bado walikuwa hawana mtoto hadi kwenye uzee wao. Hakuna kumbukumbu yeyote katika hesabu ya hawa wazazi kwamba waliwahi kutubu au kukiri makosa yao walipokuwa wakiomba miujiza kwa ajili yao. Ujumbe wa Mungu kwa wazazi hawa hautaji sababu yeyote kwamba hawakuwahi kuwa na watoto tayari. Matukio haya yanaonyesha ukweli kwamba watu hawapaswi kulaumiwa binafsi kwa ajili ya kutopata au kukosa watoto.
Inafaa sana kwa ajili yetu tuombe kwamba Mungu atatupa baraka za watoto, lakini mwishowe, ni lazima tukubaliane na uamuzi wa Mungu. Hatupaswi kudhania kwamba ni mapenzi ya Mungu atoe mtoto kwa kila hali, kama vile pia ambavyo Mungu hafanyi uponyaji kwenye kila hali ya ugonjwa au kuchukua kila aina ya mateso.
Mtume Paulo aliomba mara tatu kuhusu kitu ambacho alisema ni kama mwiba katika nyama za mwili wake (2 Wakorintho 12:8-10). Hatujui ni tatizo gani mahususi alilokuwa nalo, lakini inavyoonekana ilikuwa ni tatizo la kimwili. Ilikuwa ni kitu ambacho alimtegemea Mungu kwamba kingebadilika, kwa hiyo aliomba kwa ajili ya muujiza wake. Mungu alimjibu kwamba badala ya kumwondolea huo mwiba wake, atampa neema ambayo ingekuwa kubwa kuliko udhaifu aliokuwa nao. Paulo alisema kwamba udhaifu huu mahususi ungemletea Mungu utukufu kwa sababu ulimsaidia yeye kuonyesha nguvu ya Mungu. Paulo aliendelea kusema kwamba anapendezwa na madhaifu na mateso kwa sababu vinaleta hali ambayo itamletea Mungu utukufu.
Mtume Paulo alikuwa mtu wa imani kubwa, lakini siyo kila wakati alikuwa anapata miujiza aliyokuwa anahitaji. Alikubaliana na mapenzi ya Mungu. Ingawaje tunataka tupate muujiza wa baraka kutoka kwa Mungu, ni lazima tukubaliane na maamuzi ya Mungu. Wakati mwingine Mungu hujipatia utukufu zaidi katika njia ile anayoitumia kufanyia kazi kupitia madhaifu yetu.
► Toa mfano wa muda ambao Mungu alionyesha kukuhudumia katika maisha yako bila ya kukufanyia muujiza uliokuwa ukiutegemea.
Tamaduni zote hazifanani kwa jinsi wanavyowathamini watoto. Katika baadhi ya nchi, familia zinataka ziwe na watoto wengi. Watoto wanaweza wakasaidia katika kazi ambazo zinategemeza familia. Jamii inayounganishwa katika familia – binamu, wajomba, na wengineo huwalinda na kuitunza jamii wakati inapohitajika. Kila mke kwenye jamii inayounganishwa kifamilia hutaka kuiongeza familia kwa kuwa na watoto. Mume mwenye watoto wengi, hasa wa kiume, ni muhimu kwenye jamii inayounganishwa kifamilia. Familia hiyo inategemea kutunza wanafamilia wazee walioko.
Katika nchi nyingine, familia nyingi zinaishi kwenye majiji na miji na zinawezeshwa kimaisha na ajira ya baba na mama. Katika majiji, watoto hawana uwezo wa kuiwezesha familia kimaisha. Kuwawezesha na kuwapa elimu watoto kunaweza kuwa ni kwa gharama sana. Baada ya muda mrefu, jinsi familia zitakavyokuwa zinaendelea kuishi kwenye jiji kwa vizazi kadhaa, wanaweza wakawa wanataka kuwa na idadi ndogo sana ya watoto. Familia nyingi zinazoishi kwenye maeneo ya mijini zinataka mtoto mmoja au wawili tu.
Thamani ya watoto ni nzito sana katika tamaduni nyingi kiasi kwamba kila wanandoa ni lazima wawe na watoto ili wajisikie kwamba wanaheshimika na kuthaminika. Mwanamke ambaye hajajaliwa kuwa na mtoto hujisikia kwamba ni mwenye kushindwa katika jukumu lake muhimu la kuzaa. Mwanamke ambaye kamwe hajaolewa hujisikia mwenye aibu kwa sababu ya kutokuwa na watoto na kwamba alikuwa hajachaguliwa kuwa mke wa mtu.
Katika tamaduni nyingi familia huwa zinataka kuwa na watoto wengi wa kiume kwa ajili ya kuongoza na kuimarisha familia kwa vizazi vingine vinavyofuata. Wasichana wanathaminiwa kwa kiwango kidogo sana. Watoto wachanga wa kike wanaojulikana kabla ya kuzaliwa aidha huweza mimba kutolewa au wakatupwa wakishazaliwa. Baadhi ya nchi zimepiga marufuku kujua kabla ni jinsia gani ya mtoto ambaye hajazaliwa kabla ya wakati wake, kwa sababu familia nyingi sana huuwa vichanga vya kike ambavyo bado havijazaliwa. Tunajua kutokana na maandiko kwamba wasichana wana heshima na thamani sawa na ile waliyo nayo vijana wa kiume kwa sababu wote wameumbwa katika sura ya Mungu (Mwanzo 1:27). Kwa hiyo familia zinazomfuata Kristo zinapaswa kuwathamini kwa usawa unaolingana vijana wa kike na wa kiume haijalishi kuna jambo gani la kawaida katika tamaduni.
Ikiwa familia ina uhitaji mkubwa wa kujivunia mtoto, wanaweza wakamkataa mtoto mlemavu kimwili au kiakili. Kwenye baadhi ya nchi, watoto wengi walio na ulemavu wako kwenye vituo vya kulelea watoto yatima kwa sababu wazazi wao hawakuwataka. Utendaji huu kwa watoto ni mbaya, kwa sababu wameumbwa kwa mfano wa Mungu na ni wa thamani mbele zake, bila kujali uwezo wao au mipaka yao.
Katika baadhi ya tamaduni, desturi ya ndoa zaidi ya mke mmoja inategemea na thamani ya watoto. Mwanamume atataka kuwa na watoto wengi kwa kuwa na wanawake kadhaa. Biblia inatuambia sisi kwamba mpango wa Mungu ni mwanamume mmoja awe na mke mmoja (Mwanzo 2:22-24, 1 Timotheo 3:2).
Agano la Kale lina kumbukumbu ya nyakati kadhaa ambazo mwanamke anampa mumewe mjakazi wake ili aweze kujipatia watoto naye. Mke alipata hadhi yake kutoka kwa watoto wa mjakazi. Raheli na Leya, wake zake Yakobo, kila mmoja alimtoa mjakazi wake akampa Yakobo ili wajipatie hadhi kupitia kuwa na watoto wengi.
Matumizi ya wajakazi kwa ajili ya kuongeza watoto kulisababisha kuwepo na mahusiano yaliyokuwa na utatanishi mkubwa. Sarai alimkabidhi Hajiri kwa Abrahamu, akitarajia kwamba hadhi yake mwenyewe ingekuwa bora zaidi kama Hajiri angempatia mtoto (Mwanzo 16:2-6). Hajiri akabeba mimba na akajisikia sana kuwa yuko juu ya Sarai. Sarai alimwadhibu vikali Hajiri kwa kujaribu kujiona kwamba yuko juu zaidi yake na kuanza kujitengenezea mamlaka yake mwenyewe.
Lelia alikuwa amezaliwa katika nchi moja ya Afrika Magharibi. Baada ya kuwa ameolewa kwa miaka mitatu akawa hakujaliwa kupata mtoto. Kwa mujibu wa utamaduni wa Lelia, kuasili mtoto hakuondoi aibu ya mwanamke ya kutokuwa na mtoto wake mwenyewe. Lelia alimpata mwanamke fulani kutoka katika familia maskini kijijini ambaye alikuwa mjamzito na akapanga amnunue mtoto wake. Lelia alivaa kitu fulani ndani ya shati lake ili aonekane mjamzito kwa miezi kadhaa. Ilipofikia wakati wa mtoto kuzaliwa, Leila alijifanya kwenda hospitalini kwa ajili ya kujifungua, kisha akarejea tena nyumbani akiwa na mtoto wake aliyetoka naye kijijini.
Kama familia kimsingi inataka watoto kwa ajili ya faida yao kwa familia, wanaweza kushindwa kumthamini mtoto kama aliyeumbwa katika sura yake Mungu. Wanaweza wakakataa kuwapenda na kuwapokea watoto walemavu. Wanaweza wakamkataa mtoto wa kike kwa sababu walikuwa wanataka mtoto wa kiume. Wanaweza kumfanya mwanamke ambaye hajajaliwa kupata mtoto ajione ni wa aibu na asiyekuwa na thamani. Hawaoni thamani ya kuasili watoto yatima au watoto wasiokuwa na maskani. Tabia zote hizi na matendo haya yote ni ya kibinafsi na ni makosa. Tunamdhalilisha Muumbaji wetu tunapokuwa tunawatendea ubaya watu binafsi kwa sababu yeyote ile iliyoko hapa (Kutoka 4:11, Mithali 14:31).
Henry VIII alikuwa ni mfalme wa Uingereza kuanzia mwaka 1509-1547. Alikuwa ametarajia sana kuwa na mtoto wa kiume. Kwa kuwa mke alikuwa na binti lakini hakuwa na mtoto wa kiume aliye hai, Henry alimtalaki mkewe na kuoa mke mwingine. Mke wake wa pili aliposhindwa pia kumpatia mtoto wa kiume, alimshutumu na kumshitaki kwa makosa ya uhaini, na akaamrisha anyongwe.
Sayansi ya tiba imethibitisha kwamba manii ya kiume ndiyo huamua jinsia ya mtoto. Mwili wa mwanamke haufanyi maamuzi kama aidha atapata mtoto wa kiume au wa kike. Hata hivyo, wanaume wengi wamekuwa na hasira dhidi ya wake zao kwa sababu ya kuwa na watoto wa kike na siyo wa kiume.
Mwanamume mmoja aliyeitwa Yusufu na mke wake walikuwa na watoto wawili wa kike. Wakati mke wake Yusufu alipokwenda hospitali kwa ajili ya kujifungua mtoto wake wa tatu, Yusufu alitarajia kupata mtoto wa kiume. Mtoto wa tatu aliyezaliwa pia naye alikuwa wa kike. Yusufu alipandisha hasira sana kiasi kwamba alikataa hata kwenda hospitalini kumtembelea mke wake na kulipa gharama za matibabu.
Katika Ayubu 24, Ayubu ametoa maelezo marefu kuhusu matendo ya mtu mwovu. Tendo moja lililotajwa ni kwamba mwanamume mbaya humtendea ubaya mwanamke asiyekuwa na mtoto (Ayubu 24:21). Mungu hapendezwi pale mwanamke asiyekuwa na mtoto akitendewa mambo yasiyofaa na yasiyokuwa na upendo.
► Je, ni kwa jinsi gani utamaduni wa kwenu unawathamini watoto? Je, ni sababu zipi zinazofanya watu watake kupata watoto?
► Je, ni mambo gani ya udhalimu ambayo hutokea kwa sababu ya mila au desturi zilizoko kwenye utamaduni wenu?
Kwenye masimulizi sita yaliyorekodiwa katika Maandiko wakati Mungu akiwa anatoa mtoto wa kiume kwa mwanamke asiye na mtoto, wazazi hawakulaumiwa kwa njia yoyote kwa kukosa mtoto hapo awali. Kwa kweli, wanandoa hao walichaguliwa hasa na Mungu kuwa wazazi wa watoto wa kiume pekee. Zakaria na Elizabethi waliitwa wenye haki (Luka 1:5-6). Hatupaswi kamwe kudhani kwamba mwanamke hana mtoto kwa sababu hajampendeza Mungu.
Ayubu 24:21 anasema kwamba kumtendea vibaya mwanamke mgumba ni kitendo cha mtu mwovu. Mungu hamhukumu wala kumtendea vibaya mwanamke mgumba, na sisi pia hatupaswi tufanye hivyo.
Katika Isaya 56:4-5 Mungu anazungumza na mtu asiyeweza kuzaa watoto. Mungu anasema kwamba ikiwa mtu huyu atamtii Mungu na kuishi katika agano lake, atakuwa na nafasi na sifa ambayo ni bora kuliko ambayo angekuwa nayo kutokana na kupata watoto wa kiume na wa kike.
Mtume Paulo alijiita mwenyewe baba yake na Timotheo (1 Timotheo 1:2) na Tito (Tito 1:4) na Onesmo (Philemoni 10). Akajiita tena mwenyewe baba wa waumini wa Korintho (1 Wakorintho 4:15). Hakuwa baba yao wa kibiolojia, lakini alikuwa ni baba wa kiroho. Kuwa baba wa kiroho kulikuwa ndiyo jambo muhimu zaidi.
Mathayo 12:46-50 inatuambia juu ya wakati ambapo mama na ndugu zake Yesu walikuja kumwona akiwa anafundisha. Yesu aliwauliza wasikilizaji wake, “Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni akina nani? Baadaye akawaambia kwamba, “Ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.” Tunatambua kwamba Yesu alijali sana kuhusu familia yake; hata alipokuwa pale msalabani alipanga kuhusu utunzaji wa mama yake (Yohana 19:26-27). Lakini Yesu anasema kwamba familia ya kiroho ni muhimu zaidi kuliko familia ya kibiolojia.
Familia yenye imani haiwezi ikawa mbadala wa familia ya kibiolojia, lakini nafasi ya mtu katika familia ya imani inaweza kumpa mwanamume au mwanamke utambulisho ulio muhimu zaidi. Maneno haya kaka na dada yanayotumika katika kanisa yanaonyesha umuhimu uliopo wa mahusiano ya familia ya imani (Wakolosai 1:2).
Debora alikuwa nabii wa kike aliyehudumu kama mwamuzi kwa ajili ya Israeli (Waamuzi 4:4). Debora pia aliongoza taifa la Israeli katika vita vya kutafuta uhuru wao kutoka katika taifa lililokuwa la uonevu. Katika Waamuzi 5:7 Debora alijiita mwenyewe mama wa Israeli. Biblia kamwe haijawahi kuwataja watoto wa kibiolojia wa Debora, lakini alikuwa mama kwa ajili ya Israeli kwa sababu aliwajali watu kwa uongozi wake.
Mtume Petro alisema kwamba wanawake wanaofuata mfano wa Sara ni watoto wake. Jaribu kufikiria hadhi kubwa hivyo anayopewa Sara kwa tamko hilo! Hii ni hadhi iliyotokana na mfano wake wa imani na utiifu, na siyo kwa ajili ya jukumu lake kama mama wa Isaka.
Watu wote ambao wameokolewa kwa neema kwa njia ya imani wanaitwa wana wa Abrahamu (Wagalatia 3:7). Abrahamu anapewa heshima ya hali ya juu kabisa kama baba wa mamilioni ya watu wote walioamini/waliookoka. Kutokana na mifano ya Abrahamu na Sara tunaweza kuona kwamba Mungu kwa kiwango cha juu anaheshimu ubaba na umama wa kiroho.
Mtume Paulo alielezea faida za mtu kuwa mseja. Mtu mseja anaweza kuzingatia kumpendeza Mungu bila ya kuwepo na majukumu mengine mengi (1 Wakorintho 7:32-35). Ingawaje mtu mseja hana mtoto, Paulo alisema kwamba useja ni mzuri tu kama mtu anaweza kuishi maisha ambayo ni ya usafi. Kwa sababu ya matamko haya, tunaweza kuwa na uhakika kwamba useja ni mapenzi ya Mungu kwa baadhi ya watu.
Kama ilivyo katika useja, pia kuna faida za kutokuwa na mtoto. Kama vile Mungu alivyo na nafasi mahususi kwa wale ambao ni waseja, kadhalika anazo nafasi mahususi kwa ajili ya wale waliooana lakini hawajajaliwa kupata watoto. Ingawaje hawakuwahi kuchagua wakae bila ya kuwa na watoto, wanapaswa wafanye jitihada zote nzuri za kufanya kazi kwa ajili ya Mungu.
Kwenye useja au ugumba, na hali yeyote ile tuliyo nayo, tunaweza kumwamini Mungu kwamba atafanya kazi kupitia kwetu kwa ajili ya kutuletea sisi faida za kiroho na kwa watu wengine (Warumi 8:28).
Kuna watoto wengi ambao hawana wazazi wa kuwatunza au kuwajali. Kuna uwezekano mkubwa kwamba hakuna mtu wa kuhudumia hitaji hili maishani mwao isipokuwa pawepo na baadhi ya watu binafsi au wanandoa katika familia ya imani wafanye juhudi za ziada za kuonyesha upendo kwao.
Tumeitwa ili tuitoe miili yetu iwe dhabihu iliyo hai kwa Mungu, na tuishi kama moyo wa ibada kwa Mungu (Warumi 12:1).
1. Watoto ni baraka kutoka kwa Mungu, na ni haki kwa wanandoa kuomba kwa ajili ya Mungu kuwapa watoto.
2. Ni makosa kudhania kwamba wakati wote ni mapenzi ya Mungu kufanya muujiza wa kutoa mtoto. Siyo wakati wote huchagua kutoa mtoto, kama na vile ambavyo siyo wakati wote atafanya muujiza kwa kila hitaji lingine.
3. Ni makosa kumlaumu mwanamke au mwanandoa kwa ajili kukosa watoto. Hali ya mwanadamu imeathiriwa na dhambi ya Adamu, dhambi za mababu zetu, na dhambi zinazofanyika katika jamii yetu.
4. Tunapaswa tuwapende na kuwathamini kwa uwiano ulio sawa watoto wa kiume na wa kike kwa sababu ni watu walioumbwa kwa sura ya Mungu.
5. Mtu anaweza akawa baba au mama wa kiroho ambaye ana ushawishi kwa vizazi vingi hata bila ya kuwa na watoto wa kibiolojia.
6. Mungu hutoa fursa mahususi za huduma kwa waseja na watu ambao ni wagumba.
7. Tunapaswa kujitoa kwa Mungu na kumtukuza katika hali anazotuchagulia.
Kwa bahati mbaya, makanisa kwenye maeneo mengi yamefuata tamaduni zao zaidi kuliko Neno la Mungu wakati wanashughulikia suala la kutokuwa na watoto.
Mchungaji anapaswa kuwafundisha watu wake waweze kuliona suala la ugumba/kukosa watoto kwa mtazamo wa kibiblia, hasa kama ilivyowekwa kwa muhtasari katika sehemu iliyotangulia.
Ikiwa mchungaji anaombea muujiza kwa wanandoa wasio na watoto, haipaswi kuweka jukumu la imani kwa mke au mume. Yesu alipomponya mtoto mdogo au kufufua wafu, mtu aliyeponywa au kufufuliwa hakuwa na imani kwa muujiza wake mwenyewe. Ikiwa mchungaji ana uhakika kwamba Mungu anataka kufanya muujiza huo, mchungaji anapaswa kuwa na imani na asimlaumu mke au mume kwa ukosefu wa imani.
Katika Warumi 12:15, tunaambiwa tulie pamoja na wale wanaolia. Mchungaji anapaswa kufahamu huzuni ya watu katika kusanyiko lake. Anapaswa kuchukua hatua ya kuwatia moyo na kuwafariji wale wanaoomboleza kwa sababu ya kukosa watoto au kufiwa na mtoto. Mwanandoa pia hupatwa na huzuni wakati kichanga chake kinapokufa kabla ya kuzaliwa na ambaye hakuwahi kuishi. Kumbuka kwamba mume na mke wanateseka kwa pamoja, ingawaje watakuwa wanaonyesha hali zao kwa njia tofauti. Mchungaji asingojee watu walio na huzuni waje kwake ili kupata ushauri. Mchungaji anapaswa kufundisha kusanyiko lake kuhusu kutiana moyo na kusaidiana kila mmoja na mwenzake.
Mchungaji anapaswa aliongoze kundi katika kujenga mahusiano na kuwatunza wanandoa wazee au watu binafsi ambao bado hawajajaliwa kupata watoto. Wanafamilia wa imani wanapaswa wawachukulie kama ni wazazi, au mababu na mabibi kwa kuonyesha upendo wao, kuchukua muda wa kuwa pamoja nao, na kuwasaidia katika mahitaji yao ya msingi.
Mchungaji anapaswa awasaidie waseja na watu ambao bado kupata watoto wapate njia nzuri za kutumika na kulibariki kanisa na jamii. Mchungaji anapaswa kuthibitisha umuhimu wa kila mtu katika familia ya imani.
► Je, ni kwa jinsi gani watu katika utamaduni wa kwenu wanawachukulia watoto? Je, ni ka jinsi gani wanawachukulia wagumba na au watu ambao hawajawahi kupata watoto?
► Je, waumini katika utamaduni wako wana mtazamo gani kuhusiana watoto? Je, waumini katika utamaduni wako wana mtazamo gani kuhusu kutokuwa na watoto?
► Je, ni kwa jinsi gani uelewa wako kuhusu utasa/ugumba umebadilika au kupinga kwa kujifunza kanuni za kimaandiko zilizowasilishwa katika somo hili?
► Je, kuna wanandoa wowote ambao inawezekana wanapambana na hali ya utasa ndani ya familia yako ya imani ya kanisa? Kama ndivyo, ni kwa jinsi gani kanisa lako linaweza kuwa kuunga mkono na kuwapa sehemu salama kwa ajili ya kushirikisha mapambano yao?
Baba wa Mbinguni,
Asante kwa ajili ya familia za Kikristo. Asante kwa ajili ya waume na wake ambao wanaishi kwa ajili yako, na kwa mchango wao katika ufalme wako.
Tunaomba kwa ajili ya wale wanandoa ambao wanapambana na utasa. Tunaomba kwamba uwafariji na uwatie moyo ndani ya mioyo yao. Wasaidie katika kujua kwamba upendo wako kwao ni endelevu na usiokoma hata katika kukosa uwezo wa kupata watoto.
Ikiwa ni mapenzi yako kwao kupata watoto wa kibaiolojia, tunakuamini utafanya iwezekane kwa wakati wako. Aidha Iwe umewapa au hujawapa watoto wao wenyewe, wasaidie waweze kuwa wababa na wamama wa kiroho kwa ajili ya watu wengine.
Wasaidie waumini wote kuona thamani ya kila mtu kama walioumbwa kwa sura yako.
Ameni
(1) Andika karatasi ya kurasa mbili ambamo:
Utaelezea mitazamo ya jamii yako kuhusiana na watoto na ugumba/utasa.
Utaelezea kuhusu maandiko yanayofundisha kuhusiana na watoto.
Utaelezea kuhusu maandiko yanayofundisha kuhusiana na utasa/ugumba.
Utaelezea kutoka katika kanuni za kimaandiko ni kwa nini wanandoa hawapaswi kulaumiwa kwa lolote kutokana na utasa/ugumba wao?
(2) Watie moyo wale ambao wanakabiliana na tatizo la utasa/ugumba.
Uchaguzi wa 1: Elezea kwa maandishi jinsi utakavyoweza kudhihirisha huruma na utunzaji wako kwa mtu unayemjua kwamba anahangaika katika huzuni ya kutoweza kuzaa. Kuwa mahususi katika kutaja baadhi ya mambo ambayo unaweza kuyafanya au kusema yatakayoweza kuwa baraka kwa kaka na dada yako aliye ndani ya Kristo.
Uchaguzi wa 2: Andika barua fupi ya kumtia moyo mtu unayemjua ambaye anashughulika na tatizo la utasa/ugumba. Jaribu kuelewa hali wanayoipitia. Waache wajue kwamba unajali kuhusu jinsi wanavyojisikia. Waeleze kwamba unaomba kwa ajili yao. Utakapokuwa unawapa hiyo barua fupi, uwe tayari kuwasikiliza na kudhihirisha kwao kwamba unajali kwa ajili yao kwa njia inayofaa.
Kabla ya kuendelea na Somo la 11, darasa linapaswa kujifunza na kujadili Kiambatanisho “B”. Haya ni majadiliano mafupi kuhusiana na uzazi wa mpango, na ni mada inayohusiana na ndoa na familia.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.
Questions? Reach out to us anytime at info@shepherdsglobal.org
Total
$21.99By submitting your contact info, you agree to receive occasional email updates about this ministry.
Download audio files for offline listening
No audio files are available for this course yet.
Check back soon or visit our audio courses page.
Share this free course with others