► Je, kuna ulazima wowote wa kuomba kwa ajili ya wenye dhambi? Je, ni mahali gani kwenye Bibilia tunapoagizwa kwamba tuombe kwa ajili ya wenye dhambi?
Siyo rahisi kupata aya kwenye Biblia inayosema moja kwa moja kwamba tunapaswa tuombe kwa ajili ya mabadiliko ya wenye dhambi. Kitu tunachoweza kukipata ni aya nyingi zinazotueleza kwamba tunapaswa kuomba kwa ajili ya ufanisi wa usambazaji wa injili (2 Wathesalonike 3:1, Waefeso 6:19, Wakolosai 4:4, Matendo 4:29).
Hatujui kwamba tunapaswa tuombe kwa ajili mabadiliko ya wenye dhambi pamoja na kuomba kwa ajili ya ufanisi wa usambazaji wa injili. Tunaambiwa tuombe kwa kila mtu, ikiwa ni pamoja na kuomba kwamba wenye dhambi wapate kubadilika (1 Timotheo 2:1). Tunaambiwa tujaribu kuleta watu kwenye toba, (2 Timotheo 2:25 ). na litakuwa jambo sahihi kuomba msaada wa Mungu kwenye kazi hiyo.
Wakati kanisa linapokuwa kwenye hali nzuri, uinjilisti ulionekana kutokea kwa hiari na kwa njia ya kawaida. Katika kizazi cha kwanza cha kanisa kilichoelezwa katika kitabu cha Mtendo, inaonekana kwamba kila mtu alikuwa mwenye furaha wakati wa kueneza injili.
► Mwanafunzi anatakiwa asome Matendo 2:46-47 kwa ajili ya kikundi.
Inavyoonekana, ushirika wa kanisa ulikuwa wenye nguvu sana na wenye uhai kiasi kwamba kwa njia ya kawaida sana uliweza kuwavutia watu kujiunga nao. Hali hii inatuashiria kwamba kama kanisa halina mvuto kwa watu wapya, ushirika wake siyo wenye nguvu kama ambavyo ingetakiwa iwe.
► Mwanafunzi anatakiwa asome Matendo 5:42 kwa aili ya kikundi.
Mitume na watu wengine walipata fursa nyingi za injili kila mahali na kwa watu wote. Makanisa mengine yamekuwa hayafanyi uinjilisti, na hawana uhakika ni kwa jinsi gani waanze. Hawajui namna ya kutafuta fursa kwa ajili ya injili.
► Mwanafunzi anatakiwa asome Matendo 8:1-4 kwa aili ya kikundi.
Kwa sababu ya mateso, Wakristo wengi waliondoka Yeusalemu kwenda kuishi kwenye maeneo mengine. Walishirikisha injili kwenye maeneo yote waliyokwenda. Kwao, kushirikisha injili kulikuwa ni sehemu ya maisha yao ya Kikristo.
Mabishano ya Makanisa
Unatakiwa uepukane na mashindano yanayoibuka kuhusiana na makanisa mengine mbele ya watu ambao hawajaokoka. Usijaribu kutoa shutuma kwa makanisa yao wakati unapokuwa unashirikisha injili. Watu ambao hawajaokoka hawana ufahamu wa kiroho wa kuja kwenye maamuzi sahihi kwenye mabishano ya kidini. Watu wengi wa kidunia wanasema kwamba migogoro iliyoko miongoni mwa makanisa ni sababu za wao kutoamini katika Ukristo.
Kama mtu ataweka msisitizo kwenye kuulizia kuhsu tofauti za kiimani, mpatie majibu kutoka kwenye maandiko, lakini jaribu kumrejesha kwenye kipaumbele cha injili. Unaweza kusema, “Maswali kama hayo ni muhimu, lakini jambo muhimu zaidi ni kuokoka na kuwa kwenye uhusiano na Mungu.” Kama watakuelezea kuhusu Mkristo waliyemjua, labda mtu katika jamii au mchungaji, jaribu kutoelezea mambo ya lawama kuhusiana na imani ya mtu huyo.
Kama una kitu cha kuelezea ni kwa nini kanisa lako ni tofauti na kanisa lingine, unaweza ukasema, “Ni muhimu kwa mtu kutubu dhambi zake, akasamehewa, na akaishi kwenye maisha ya utiifu kwa Mungu. Makanisa yetu huwekea mkazo kipaumbele hicho, kwa hiyo tuko tofauti na makanisa mengine yaliyo na msisitizo wa mambo mengine.”
Maswali Magumu
Baadhi ya Wakristo wana hofu ya kufanya uinjilisti kwa sababu wanahofia kuulizwa maswali magumu. Ni vyema kuendelea kujifunza, lakini ukweli ni kamba wakristo wengi hawajui jinsi ya kujibu maswali yote magumu. Hauhitaji kujua majibu ya maswali yote.
Kama mtu atakuuliza swali ambalo unaliona ni gumu kuweza kujibu, unaweza ukasema kama ifauatavyo: “Sijui jibu sahihi kwa swali lako. Kuna mtu kwenye kanisa letu anaweza akasaidia kujibu swali hilo. Lakini mimi ninaiamini Biblia, na jambo muhimu zaidi ninaloliamini ni kumjua Mugu na kuokoka. Ninajua ni kwa jinsi gani unaweza kufanya ili uokoke.”
Kama mtu atasema, “Mimi siiamini Biblia,” au “Mimi siamini katika Mungu,” kuna mielekeo miwili tofauti unayoweza kuitumia kuelekeza mazungumzo hayo. Unaweza ukamwuliza sababu iliyo katika mawazo yake na ukajaribu kumpa baadhi ya ushahidi ulio nao. Mwelekeo mwingine ni kusema, “Inaelekea ulikuwa na wazo katika hili na ukajaribu kuja kwenye uamuzi wenye maana. Lakini hata kama huiamini Biblia, kama mtu mwenye busara unatakiwa kujua ujumbe wa msingi wa Biblia. Je, ninaweza kukuonyesha ni kitu gani?” Kwa kufanya hivi, unaweza ukajikuta unashirikishana injili pamoja naye bila ya kushindana. Mungu anaweza akautumia ujumbe huo katika kugusa maisha yake kwa wakati wa baadaye.
Wakati unapokuwa unapofanya uinjilist, unaweza kukutana na mtu ambaye nia yake anataka tu ashindane na wewe. Unapaswa uepuke kupoteza muda mwingi na mtu wa aina hii. Hata kama utasema mambo yote yaliyo sahihi, inawezekana asikubaliane na ukweli wako. Jaribu kumshirikisha misingi ya injili kisha ondoka hapo ukazungumze na mtu mwingine.
Kuitetea Injili
► Soma Tito 1:9-11. Je, aya hii inatoa sababu gani kwamba sisi tunapaswa tuilinde injili?
Mojawapo ya uwezo ambao mchungaji anapaswa kuukuza ni uwezo wa kuulinda ukweli wa Ukristo dhidi ya falsafa za dunia. Hii haina maana ya kuzungumzia kuhusa ushindani wa imani za makanisa tofauti, bali ukinzani wa dunia dhidi ya injili.
Sababu ya kutufanya tuutetee ukweli siyo tu kwa sababu ya kutaka kumbadilisha mtu anayeshindana, bali kuwasaidia watu ambao wanavutiwa na yeye. Watu wengi bado hawajawa na uamuzi wa kitu gani cha kuamini. Wanahitaji kusikia utetezi wa ukweli wa Kikristo.
Wakristo wengi bado hawajajazwa kwa ukamilifu uwezo huu wa kufanya aina hii ya ushindani. Kila Mkristo anatakiwa ajifunze kwa kadri inavyowezekana, lakini kuna baadhi ambao wamejaliwa karama hii na wako tayari kwa ajili ya kazi hiyo.
Wakati wa ushindani, ni muhimu sana kuonyesha kusudi lako. Hauko hapo kwa kujaribu kushinda mashindano. Haupambani na mtu kama adui yako binafsi. Unapaswa uonyeshe kwamba ukweli ni muhimu kwako kwa sababu unawajali watu. Kama hataiamini injili, roho yake itapotea. Ndio maana uko hapo kwa kusudi la kutaka kubadilisha ufahamu wake. Unaweza ukasema jambo lolote kama, “Ninakutaka wewe umfahamu Mungu na uokoke, na nina wasiwasi kwamba unaamini kitu ambacho hakitaweza kukupeleka kwa Mungu.”
Kukuza ujuzi wa Kutengeneza fursa
Tunazo kumbukumbu katika nyakati za Biblia ambapo mwinjilisti alitafuta nafasi maalumu kwa ajili ya kushirikisha injili.
► Mwanafunzi atapaswa asome Matendo 8:26-39 kwa ajili ya kikundi. Mwanafunzi mwingine anaweza akaulizwa kufanya muhtasari wa maelezo kwa ajili ya kikundi. Je, ni kwa jinsi gani Roho wa Mungu aliwajibika kwenye hili tukio? Ni kwa jinsi gani Filipo aliitambua fursa iliyojitokeza kwa ajili ya injili?
Mfano mwingine wa mwinjilisti kutambua nafasi inayojitokeza kwa ajili ya injili ni Yesu mwenyewe.
► Mwanafunzi atapaswa asome Yohana 4:7-14 kwa ajili ya kikundi. Mwanafunzi mwingine anaweza akaulizwa kufanya muhtasari wa maelezo kwa ajili ya kikundi.
Mazungumzo haya kati ya Yesu na mwanamke Msamaria yalihusisha pamoja na mada za migogoro ya kimila, utata wa kidini, na mfumo mzima wa maisha. Yesu hakuchukua muda mrefu katika mada hizo, lakini aliyaongoza mazungumzo yake kwenye mada ya mahitaji ya kiroho ya yule mwanamke.
Utakapokuwa umejifunza jinsi ya kuwasilisha injili, utatafuta nafasi za kushirikisha watu wengine. Mara chache, mtu anaweza akataka kuisikia injili, lakini nafasi kama hiyo haiko wazi hivyo.
Baadhi ya Wakristo huhisi kwamba ni vigumu kushirikisha injili kwa sababu wanadhania kwamba watu hawana haja ya kusikiliza. Wanafikiri kwamba ni vigumu kuanzisha mazungumzo yanayohusiana na dini.
Injili huhusika na mambo mengi waliyo nayo watu. Kwa hiyo, hakuna tatizo la kuanza kuzungumzia injili katikati ya mazungumzo yanayoendelea.
Katika somo hili, baadaye tutazungumzia kuhusu sababu wanazokuwa nazo watu hata kutamani injili.
Aina mbali mbali za dhamira
Watu wana aina nyingi za sababu za kuupokea wokovu. Wakati mwingine kunakuwepo na dhamira mbaya, lakini kuna sababu nyingi za dhamira sahihi.
► Je, kulikuwa na sababu gani zilizokufanya wewe ukakubaliana na injili? Toa nafasi kwa wanafunzi waeleze sababu zao wenyewe zilizowafanya wakakubali kuokoka.
Hapa kuna aina nyingi dhamira ambazo zinawafanya watu wahitaji kuokoka.
Kwenda mbinguni na siyo motoni (au hofu ya hukumu)
Kuwa na utimilifu na kusudi katika maisha
Kuwa na ulinzi, amani ya rohoni, na kuwa huru kutokana na hofu
Kupata msamaha, uhuru wa kutokuwa na hatia (dhamira iliyo wazi)
Kuwa msafi kiroho na katika mambo yote
Kuwa na ushirika na Mungu (kumjua Mungu)
Kuwa na ushirika na Wakristo wengine
Kuwa na utoshelevu wa matamanio ya kiroho (furaha ya kweli)
Kupokea ukombozi kutokana na dhambi
Kuujua ukweli
Haya ni mafanikio ya moja kwa moja ya upatanisho na Mungu. Siyo mambo ya kidunia ambayo yanapingana na thamani za umilele. Mtu anakosa vitu hivi kama anakuwa ametengwa na Mungu.
► Angalia kwenye orodha hii na jaribu kutafakari ni vitu gani ambavyo ni muhimu kwako. Ni vitu gani vilikuvutia wewe kabla hujabadilishwa na kuokoka? Ni vitu gani ambavyo vilikuwa ni vya muhimu sana kwako baada ya kubadilishwa na kuokoka?
Mtu ambaye hajaokoka anaweza akaonesha kwenye mzungumzo yake kwamba anajisikia kuhitaji mojawapo ya manufaa haya ya kuokoka. Mwinjilisti anaweza akabadilisha njia yake aliyokuwa anaitumia kuwasilisha injili ili kushughulika na hitaji hili. Sema, “Sababu ambayo watu hawana ______ ni kwamba wametengwa na Mungu. Biblia inatuambia jinsi ya kurejea tena upya kwenye uhusiano na Mungu.”
Ni muhimu kuhakikisha kwamba hatutoi ahadi za furaha ya dunia kwa mtu yeyote ambaye anataka kuwa Mkristo. Mtu ambaye anaamua kuwa Mkristo, kwa sababu hiyo inawezekana siyo wa kutubu dhambi yake kwa ukweli, na, kwahiyo, hataweza kupata haya mafanikio ya kuokoka. Sababu nyingine zinazotufanya tusitoe ahadi za furaha ya dunia ni kwamba Biblia haitoi ahadi ya hali zilizo nzuri kwa Wakristo; badala yake, inatabiri mateso (2 Timotheo 3:12).
Sababu kubwa na ya muhimu inayomfanya mtu kutaka kuwa Mkristo ni kwamba anajitambua ni mwenye hatia na kwamba kuna hukumu inayokuja. Vitu vingine vilivyoko kwenye orodha hapo juu vinaweza kutumika kumsaidia mtu katika kujitambua kwamba ametengwa na Mungu.
Kutambua Nafasi Zinazojitokeza kwenye Mazungumzo
► Je, ni upenyo gani umewahi kuutumia katika kupata nafasi ya kushirikisha injili?
► Je, imeshawahi kutokea ikaoneakana ni vigumu kwa yeyote kati yenu kupata nafasi ya kushirikisha injili? Je, Unafikiri ni kwa sababu gani?
Mara nyingine nafasi inaweza ikajitokeza kwa urahisi. Kwenye hali kama hiyo, unaweza tu kirahisi kuanza kuelezea kuhusu injili. Kama utataka uwaonyeshe aya za maandiko, unaweza ukawauliza, “Je, ninaweza nikatumia dakika chache kuwaonyesha kile ambaco Biblia inasema kuhusiana na jinsi ya kuwa Mkristo? Kama utataka kuonyesha daraja la mchoro, unaweza ukawauliza, “Je, ninaweza kuchukua dakika mbili kuwaonyesha mchoro ambao unaoelezea kile ambacho Biblia inasema kuwa ni njia ya kujua kwa uhakika kwamba umeokoka?”
Upenyo hujitokeza katika mazungumzo kwenye namna nyingi za mada. Kwa upenyo wowote unaotokana na mazungumzo ulioelezewa hapa unaweza kutumika kwa ajili ya kuwasilisha daraja la mchoro au kuwasilisha injili kutoka kwenye Maandiko kama vile Barabara ya Kirumi.
► Je, ni watu wengi kiasi gani mmeshasikia wakilalamika kuhusu hali ngumu ya maisha yao?
Mara nyingine watu hulalamika kuhusu hali ngumu katika maisha yao. Waulize, “Je, Kwa nini maisha yamekuwa magumu kiasi hicho?” Baada ya kukujibu, sema, “Je, ninaweza kuwaonyesha mchoro ambao unaelezea ni kwa nini maisha yamekuwa magumu kiasi hicho?” Anza kwa kusema kwamba Mungu alitukusudia sisi tuishi kwenye mahusiano pamoja naye na hajakusudia kwetu maisha yawe magumu kama yalivyo sasa. Dunia imeharibiwa na dhambi. Kisha endelea na uwasilishaji wa mchoro.
Kutaka kuwasilisha moja kwa moja kutoka kwenye Maandiko, kama Barabara ya Kirumi, Unaweza kusema, “Biblia inafafanua kwamba maisha ni magumu kwa sababu kila mtu ametenda dhambi. Dhambi imeleta laana juu ya dunia.” Sasa, endelea kwenye Barabara ya kirumi.
Kama mtu ataonekena kuwa wa kidini zaidi, unaweza ukamuuliza imani anayoiona ni muhimu sana kwake ni ipi. Au unaweza kumwuliza, “Je, unaamini ni njia ipi ambayo mtu anaweza akajua kwamba ataingia mbinguni?” Baada ya kusikia jibu lake, mwulize, “Je, ninaweza kuchukua dakika mbili za kukuonyesha mchoro ambao unaelezea kile ambacho Biblia inasema kuhusiana na jinsi mtu atakavyoweza kuingia mbinguni?”
► Je, umeshawahi kusikia watu wakizungumzia kuhusu hali mbaya ya dunia au matatizo ya kitaifa? Ni kwa jinsi gani utaweza kutumia hali hizi kama upenyo wa nafasi ya kushirikisha injili?
Kama mtu anazungumzia kuhusu matatizo ya kitaifa, njaa ya dunia au umaskini, au majanga ya vita, mwulize, “Je, ninaweza kukuonyesha Maandiko ambayo yanafafanua ni kwa nini dunia imekuwa kama ilivyo sasa?”
Onesha kwamba hali ya dunia iko kama ilivyo kwa sasa kwa sababu wenye dhambi wametengwa na Mungu. Usitake kuonesha kwa ujumla, kwamba kuokoka kunamaliza matatizo yote, lakini onesha kwamba kuokoka kwa mtu binafsi ni mwanzo wa suluhisho la Mungu. Siku moja kutakuwepo na mbingu mpya na nchi mpya na matatizo hayo hayataonekana tena kwa watu ambao kwa sasa wamepatanishwa na Mungu.
Kutumia Maswali ya Kufungua
Maswali yanaweza kutumika katika kuanzisha mazungumzo, na kisha mazungumzo hayo yatafungua nafasi kwa ajili ya injili.
Swali la kwanza kabisa ni kuuliza tu kirahisi kwamba “Wewe ni Mkristo?” Mara nyingi watu wengi hawakwaziki na swali hili. Kama mtu atasema, “Hapana,” unaweza ukauliza, “Je, ninaweza nikakueleza ni kwa jinsi gani mtu anakuwa Mkristo?”
Mtu huyo akisema, “Ndiyo, mimi ni Mkristo,” unaweza kusema, “Hiyo ni nzuri sana. Ulipataje kuwa Mkristo?” Kama jibu ni potofu au inaonekana mtu amechanganyikiwa, unaweza ukachagua kufafanua Biblia inasema nini kuhusiana na mtu kuwa Mkristo.
Maswali yaliyoko kwenye sehemuya hapo juu yanaweza yakatumika kama maswali mengine ya kufungua wakati wa mazungumzo. Hapa chini kuna maswali ya nyongeza.
“Unafikiri kusudi la maisha ni nini?” Acha mtu atoe maoni yake. Kubaliana na kila kitu kinachooneka ni chema katika kauli zake. Kisha utasema, “Sehemu muhimu sana katika kusudi letu ni kumjua Mungu. Alituumba sisi ili tuishi kwenye uhusiano na yeye. Je, ninaweza kukuonyesha kile ambacho Biblia inasema kuhusu jinsi ya kuwa kwenye uhusiano na Mungu?”
“Je, unafikiri msingi mkuu wa furaha ni nini?” Lolote litakalojibiwa, unaweza kusema, “Watu wengi walio na furaha hawaonekani kuwa na furaha kwa muda mrefu. Biblia inatuambia kwamba furaha inatoka kwa Mungu (Zaburi 16:11). Je, ninaweza kuwaonyesha mchoro ambao unaelezea ni kwa jinsi gani mtu anaweza akawa kwenye uhusiano na Mungu?”
“Je, unaamini kwamba kuna maisha mengine baada ya kufa? Unadhani yanafananaje?” Kisha, “Biblia inasema kwamba kila mtu aidha ataingia mbinguni au ataingia motoni. Je, ninaweza kukuonyesha kile ambacho Biblia inasema kuhusu jinsi ya kuingia mbinguni?”
“Je, unadhani msingi mkuu wa ujumbe wa Biblia ni nini?” Hapa inakupa wewe nafasi ya kuonyesha mchoro ulioko katika somo la 9.
► Je, kuna mtu yeyote miongoni mwenu ambaye tayari alishawahi kutumia njia inayofanana na mojawapo katika hizi? Ilifanyaje kazi?
Siyo kila mwanafunzi atajisikia vyema na mbinu zote ambazo zimeelezwa katika somo hili. Inawezekana kabisa kwamba mbinu mojawapo isionekane inafaa katika kila mila.
Kusudi la somo ni kumsaidia mwanafunzi kutafuta jinsi ya kukuza upeo wake wa njia zake mwenyewe za kuwasilisha.
Ukumbusho kwa Kongozi wa Darasa
Somo linalofuata limehusisha maelekezo kwa ajili ya kusambaza vipeperushi. Wanafunzi watahitaji kujua ni mahali gani wanatakiwa wapate hivyo vipeperushi kwa ajili ya kuvisambaza. Kama itawezekana, njoo na vipeperushi vya kusambaza kwenye kipindi kingine cha darasa kitakachofuata.
Kazi ya Kufanya
Utakapokuwa unaendelea kuwasilisha injili katika wiki hii, jaribu baadhi ya haya maswali ya kufungua mazungumzo au andaa yako mwenyewe. Fanya kuangalia kwa makini ni kwa jinsi gani yanafanya kazi na andika aya moja kuelezea haya. Uwe tayari kueleza uzoefu wako ulioupata kwenye kipindi kingine cha darasa kitakachofuata.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.